Schröder ziarani Iran
23 Februari 2009Baraza la Wayahudi nchini Ujerumani limemkosoa kansela huyo wa zamani wa Ujerumani kwa sababu ya kukutana na Ahmadinejad.Hapo mwanzoni,ziara hiyo ya siku nne ya Schröder nchini Iran ilipangwa kuwa ya binafsi.Alialikwa na rafiki yake alie daktari wa Kiirani katika mji wa Hannover,kaskazini ya Ujerumani.Schröder mjini Tehran,alishiriki katika sherehe za kufungua taasisi ya kisayansi na kupewa jina jipya kliniki moja ya chuo kikuu.Pole pole akaanza kualikwa katika mikutano ilio na utata. Kilele chake kilifikia siku ya Jumamosi alipokutana na Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.
Schröder hakukosolewa tu na Baraza la Wayahudi nchini Ujerumani. Ahmadinejad amekanusha kutokea kwa mauaji makuu ya Wayahudi- Holocaust wakati wa utawala wa kifashisti.Nae Schröder wala hakusita kumkosoa Ahmedinejad kuhusu matamashi hayo ya ubishi. Alipohutubia Baraza la Wanaviwanda na Wafanya Biashara mjini Tehran, Schröder alieleza wazi wazi kuwa mauaji makuu ya Wayahudi ni ukweli wa kihistoria na hakuna maana kukanusha uhalifu huo usio na mfano.Akasema,Iran inahitaji kuwajibika na kuheshimu sheria za kimataifa ikiwa inataka kutiwa maanani kama taifa lenye usemi katika kanda hiyo.
Mkutano wa Schröder na Ahmadinejad vile vile umekosolewa na msemaji wa sera za kigeni wa vyama vya CDU na CSU bungeni,Eckart von Klaeden. Hivi sasa, Ahmadinejad yupo katikati ya kampeni ya uchaguzi na anatafuta njia ya kujitetea baada ya kusababisha hali mbaya mno ya uchumi nchini Iran. Kwa hivyo ni muhimu kuwa Schröder alikutana pia na mhasimu wa Ahmadinejad atakaegombea uchaguzi ujao-rais wa zamani Mohammad Khatami anaependelea mageuzi.Lakini mkutano huo haukuripotiwa katika televisheni ya Iran.
Kwa upande mwingine haijulikani iwapo Schröder,kama mshauri wa kampuni ya gesi ya Urusi-Gazprom anapigia debe uhusiano mzuri na Iran. Kwani Iran ina akiba kubwa kabisa ya mafuta na gesi duniani na mwanzoni mwa majira ya joto,kunatazamiwa kufanywa majadiliano kati Gazprom na Iran kushirikiana kuchimba gesi nchini Iran.
Serikali ya Ujerumani hadi hivi sasa haikutoa maoni yake kuhusu ziara ya Schröder-wizara ya mambo ya nje imethibitisha tu kuwa inaarifiwa juu ya kile kinachoendelea katika ziara hiyo ya Schröder.