Schweinsteiger nje ya kikosi cha Ujerumani
25 Machi 2013Schweinsteiger alionyeshwa kadi ya pili ya njano wakati wa mchuwano ambao Ujerumani ilishinda magoli matatu kwa sifuri mjini Astana Ijumaa iliyopita, na ambao alifunga goli la kwanza na atakosa mechi ya leo mjini Nuremberg.
Kocha Joachim Löw ni lazima aamue kama ataijaza nafasi yake na kiungo wa Borussia Dortmund Ilkay Guendogan jinsi ilivyokuwa katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Ufaransa mwezi uliopita. Löw pia amempa nafasi kiungo mwingine wa Dortmund Sven Bender ambaye amepona kutokana na mafua.
Ijumaa iliyopita, Ujerumani ilicheza bila mshambuliaji kwa mara ya tatu mfululizo lakini Löw huenda akataka kuipima hali ya Mario Gomez ambaye alijeruhiwa kwa miezi kadhaa mwaka jana, kama mchezaji huyo wa Munich atapona kwa wakati unaofaa kutokana na jeraha la paja.
Huku Julian Draxler akiwa nje pamoja na mwenzake wa Schalke Benedikt Hoewedes, Löw amewaita kikosini beki wa SV Hamburg Marcell Jansen na kiungo wa Borussia Moenchengladbach Patrick Hermann. Mfumo wa bila kumtumia mshambuliaji umefanya kazi vizuri kwa Wajerumani.
Katika mechi nyingine za kesho, Uhispania itakuwa na wachezaji wao mahiri wa safu ya kiungo, Xavi, Xabi Alonso na Sergio Bousquets katika kikosi chao dhidi ya Ufaransa mjini Paris. Uingereza watakabiliwa na makaribisho yenye hisia nyingi wakati watakapopambana na Montenegro.
Vettel akashifiwa kote ulimwenguni
Na katika mbio za magari ya Formula One, bila shaka kumekuwa na gumzo kila mahali tangu ushindi wenye utata wa dereva Sebastian Vettel wa RedBull katika mkondo wa Malasyia GP. Shutuma zimeendelea kutolewa dhidi ya dereva huo huku magazeti mengi yakiiangazia hatua ya kumpiku dereva mwenzake wa RedBull Mark Webber licha ya amri ya timu yake ya kutofanya hivyo.
Vettel ameomba msamaha lakini hilo halikumzuia dhidi ya matamshi yenye hisia kali kutoka kote ulimwenguni. Gazeti la Kronen Zeitung la nchini Austria, nyumbani kwa kampuni ya RedBull limeandika kichwa „je washindi hupenda hili?“
Mambo hayakuwa mazuri hata nyumbani kwa Vettel hapa Ujerumani, ambako magazeti kama The Bild yalichapisha kichwa „ushindi mchafu“ nalo Suddeutsche Zeitung likasema „Vettel sasa ni lazima aishi na sura ya kuwa mbinafsi asiyejali ambaye huikumbuka tu timu wakati itamfaidi yeye tu.“
Rais wa Kampuni ya RedBull Christian Horner ameshauriwa kuchukua hatua kali dhidi ya Vettel, ili liwe funzo katika mchezo wa Formula One.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef