Serikali ya Burundi kususia mazungumzo ya amani
28 Aprili 2016Wakati serikali ya Marekani ikihimiza maafisa wa serikali ya Burundi kuuzima mzozo huo wa mwaka mmoja taarifa kutoka ofisi ya rais iliotangazwa kwenye radio ya taifa nchini Burundi hapo Jumatano na kusikika mjini Nairobi Kenya imetowa masharti kadhaa ili serikali ijiunge na kile kinachoitwa "mazungumzo ya Burundi."
Willy Nyamwite afisa mawasiliano katika ofisi ya rais amesema serikali ya Burundi lazima ishauriwe na kwamba lazima wafikie makubaliano kuhusu watu wanaopaswa kualikwa,tarehe ya kufanyika mazungumzo hayo na mahala pa kufanyikia mazungumzo hayo.
Pia ameongeza kusema kwamba serikali inasubiri mwaliko rasmi.
Baadae ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ndio kwanza imepokea mwaliko huo wa mazunguzo ya mzozo wa Burundi yaliopangwa kufanyika Jumatatu na kwamba inauchambuwa na itajibu wakati wowote ule kwa njia zinazostahiki.
Burundi iko kwenye mfarakano wa kisiasa kwa zaidi ya mwaka mmoja ambapo watu 270,000 wamelazimika kukimbilia uhamishoni na wengine zaidi ya 500 kuuwawa.
Mkapa anaongoza mazungumzo
Mazungumzo chini ya usimamizi wa kanda kati ya Warundi wote yanashinikizwa na jumuiya ya kimataifa kama njia muafaka ya kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe na rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa anayeongoza mazungumzo hayo mwishoni mwa wiki iliopita alitangaza mazungumzo hayo mapya yatafanyika mjini Arusha Tanzania tarehe pili hadi tarehe sita Mei.
Kuanza upya kwa mazungumzo hayo kumekaribishwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku kama ni njia bora za kurudisha amani na utulivu kwa Warundi na kuwataka wadau wote washiriki mazungumzohayo bila ya kuweka masharti.
Lakini serikali mara kwa mara imekuwa ikigoma kuketi meza moja na kundi kuu la muungano wa upinzani CNARED na viongozi wa upinzani walioko ndani ya nchi na wale walioko uhamishoni ambao inawashutumu kwa kuchochea ghasia.
Masharti ya serikali
Nyamwite amenukuliwa akisema kwenye radio kwamba "wale walioshambulia maisha ya raia , wale waliotarajia kupinduwa taasisi za serikali ambazo zimechaguliwa kidemokrasia na wengine waliohusika na uasi wa kutumia silaha katika nchi yao hawawezi kuitwa kushiriki mazungumzo hayo."
Muungano wa upinzani wa CNARED umesema uko tayari kushiriki mazungumzo hayo ya Jumatatu juu ya kwamba bado haukupokea mwaliko rasmi.
Afisa wake wa mawasiliano Jeremie Minani ameitaka serikali ya Burundi itambuwe kwamba sio sehemu ya upatanishi bali ni sehemu ya mzozo kama ilivyo kwa muungano wa upinzani wa CNARED.
Amesema hawastahiki kuandaa orodha ya washiriki au kuweka agenda ya mazungumzo hayo. Mzozo wa sasa Burundi ulianza kufuatia uamuzi tata wa Rais Pierre Nkurunziza mwezi Aprili mwaka jana kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwezi wa Julai uliosusiwa na upinzani ambapo alishinda.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga