1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kenya yakosolewa kushindwa kuzuia mauaji

Mohammed Khelef6 Aprili 2015

Ulinzi umeimarishwa katika msimu wa Pasaka, huku Wakenya wakitaka majibu ya kwa nini polisi na vikosi vya usalama vilishindwa kuzuia mauaji ya maangamizi kwenye Chuo Kikuu cha Garissa mara moja.

https://p.dw.com/p/1F34g
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia taifa baada ya mauaji ya Garissa.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia taifa baada ya mauaji ya Garissa.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

Makanisa nchini Kenya yameongezewa ulinzi kwa ajili ya waumini wake katika sikukuu hii ya Pasaka, kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na watu wenye silaha katika jengo la Chuo Kikuu cha Garissa wiki iliyopita, ambayo yalipelekea mauaji ya watu 148 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wanamgambo wanne walioziba nyuso zao waliwatenganisha wanafunzi wa Kikristo mbali na wale wa Kiislamu na kisha kuwauwa wa Kikristo. Jana, Jumapili (5 Aprili), polisi wawili waliovalia sare na wakiwa na bunduki aina ya AK-47 walionekana wakilinda jengo la Kanisa Kuu la Holy Family Basilica jijini Nairobi. Asilimia 83 ya Wakenya ni Wakristo miongoni mwa raia milioni 44 wa nchi hiyo.

Mamlaka nchini Kenya zimeweka amri ya kutotoka nje wakati wa usiku katika kaunti nne zinazopakana na Somalia. Kenya ina mpaka wa kilomita 700 kati yake na Somalia. Helikota za kijeshi zimetumwa kwenye ukanda wa pwani, ambao ni mashuhuri kwa shughuli za kitalii na umekuwa ukilengwa na mashambulizi ya kundi hilo lenye siasa kali.

Watu watano wanasemekana kukamatwa wakihusishwa na mashambulizi hayo. Wanamgambo wanne waliofanya mauaji hayo ya maangamizi waliuawa na vyombo vya usalama.

Vikosi vya usalama vyakosolewa

Vyombo vya habari nchini Kenya vinavilaumu vyombo vya usalama kwa kuchukuwa muda mrefu kabla ya kutuma wanajeshi kwenye eneo hilo la mauaji. Gazeti la Nation lilisema iliwachukuwa wanajeshi kiasi cha masaa saba kufika Garissa baada ya kupokea taarifa za awali juu ya mashambulizi hayo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, vyombo vya usalama vilifika kwa mwendo wa polepole ikilinganishwa na waandishi wa habari waliotokea kwenye mji mkuu, Nairobi, umbali wa kilomita 635.

Hii ni moja ya familia zilizofanikiwa kumpata mtoto wao akiwa hai.
Hii ni moja ya familia zilizofanikiwa kumpata mtoto wao akiwa hai.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Mwenda Njoka, aliitetea kasi ya kutumwa kwa vikosi vya usalama, akisema inachukuwa muda mrefu kutathmini na kufanya maamuzi "kutoka Kamati ya Ushauri wa Usalama wa Taifa kwenda Baraza la Usalama wa Taifa na kisha kukusanya vikosi, kuvipeleka uwanja wa ndege na kuwasafirisha hadi Garissa, ambao ni mwendo wa masaa mawili kwa ndege."

Mtoto wa afisa wa serikali

Polisi ilisema siku ya Jumapili (Aprili 5) kwamba mmoja wa washambuliaji alikuwa mtoto wa kiume wa afisa mmoja wa serikali. Njoka alisema Abdirahim Abdullahi alikuwa mmoja wa watu wanne waliolivamia jengo la Chuo Kikuu cha Garissa siku ya Alhamisi.

Ndugu na jamaa wakingojea kuwatambua watoto wao waliouawa kwenye mashambulizi ya Garissa.
Ndugu na jamaa wakingojea kuwatambua watoto wao waliouawa kwenye mashambulizi ya Garissa.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

Afisa mmoja kutoka eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kijana huyo alikuwa mwanafunzi wa sheria kwenye Chuo Kikuu cha Nairobi, na kwamba alijiunga na al-Shabaab baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 2013.

"Baba yake alikuwa ameripoti kwenye vyombo vya usalama kwamba kijana wake ametoweka nyumbani .... na alikuwa akisaidiana na polisi kumfuatilia mwanawe wakati mashambulizi ya Garissa yalipotokea," Njoka aliliambia shirika la habari la Reuters. Baba yake Abdullahi ni chifu kwenye Kaunti ya Mandera.

Al-Shabaab alisema mashambulizi hayo ya Garissa, mji ulio umbali wa kilomita 200 kutoka mpaka wa Somalia, yalikuwa ni ya kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia wanaoshirikiana na walinda amani wa Umoja wa Afrika dhidi ya kundi hilo.

Mauaji hayo ya Alhamisi yalikuwa makubwa kabisa nchini Kenya tangu yale ya mwaka 1998 dhidi ya ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, na mabaya kabisa kuwahi kufanywa na al-Shabaab hadi sasa.

Mwaka 2013, wapiganaji hao walilivamia jengo la maduka la Westgate kwenye mji mkuu Nairobi na kuwauwa watu 67 baada ya kulishikilia jengo hilo kwa siku nne.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Dahman