1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Misri yapunguza saa za kutotoka nje usiku

1 Septemba 2013

Serikali ya muda ya Misri imepunguza amri ya marufuku ya kutotoka nje usiku kwa saa mbili baada ya kupungua kwa ghasia nchini humo tangu kutawanywa wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi

https://p.dw.com/p/19Zev
Picha: Mohamed El-Shahed/AFP/Getty Images)

Baraza la mawaziri la Misri limetangaza kuwa amri hiyo ya marufuku sasa itaanza saa tano usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi.Hata hivyo marufuku ya kutotoka nje Ijumaa itasalia bila mabadiliko kuanzia saa moja jioni wakati ambao mara nyingi wafuasi wa udugu wa Kiislamu huanza maandamano yao.

Watu wanane waliuawa katika maandamano ya Ijumma yaliyoitishwa na udugu wa kiislamu kote nchini humo kuipinga serikali ya mpito.Maandamano hayo hayakuwa makubwa yakilinganishwa na mwanzoni mwa mwezi Agosti na wafuasi hao wa Mursi wameamua kutumia mbinu ya kukusanyika kwa makundi madogo madogo ili kuepuka matumizi ya nguvu ya maafisa wa usalama.

Serikali wakati huo huo inaendeleza na kampeni yake ya kuwakamata viongozi wa udugu wa kislamu na maafisa wengine wa kundi hilo waliokuwa wakiandaa maandamano hayo.Jumamosi polisi ilimkamata mwanachama wa ngazi ya juu wa udugu huo Sobhi Saleh.

Polisi wa kuzima fujo wakishika doria mjini Cairo
Polisi wa kuzima fujo wakishika doria mjini CairoPicha: Reuters

Huku hayo yakijiri kiongozi mkuu wa udugu wa kiislamu Mohammed Badie anayezuiliwa na maafisa wa usalama alipata mshutuko wa moyo akiwa katika jela ya Tora viungani mwa mji mkuu Cairo.

Mohammed Badie apata mshutuko wa moyo

Gazeti la serikali al Ahram limeripoti kuwa kundi la madaktari lilitumwa katika jela hiyo kushughulikia tatizo hilo la kiafya na kuongeza kuwa mshutuko huo wa moyo unaripotiwa kusababishwa na msongo wa mawazo.Hali ya Badie inaripotiwa kudhibitiwa.

Ripoti za awali mitandaoni zilisema kiongozi huyo wa udugu wa kiislamu alikuwa amefariki gerezani kutokana na mshtuko huo lakini wizara ya mambo ya ndani ilikanusha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa facebook.

Badie anakabiliwa na mashitaka ya uchochezi na yanayohusiana na mauaji ya waandamanaji waliompinga Morsi nje ya ikulu ya rais mwezi Desemba mwaka jana na kuchochea uvamizi wa makao makuu ya jeshi la Misri baada ya kuondolewa madarakani kwa Morsi mwezi Julai mwaka huu.

Kiongozi wa udugu wa kiislamu Mohammed Badie
Kiongozi wa udugu wa kiislamu Mohammed BadiePicha: Reuters

Serikali inaushutumu udugu wa Kiisalmu kwa vitendo vya kigaidi na imepania kulitokomeza kundi hilo.Nalo kundi hilo linaishutumu serikali ya muda nchini Misri kwa kupanga njama ya kurejesha utawala wa zamani unaohusishwa na rais wa zamani Hosni Mubarak aliyeangushwa madarakani mwaka 2011.

Kukamatwa kwa viongozi wa udugu wa Kiislamu kumedhoofisha kundi hilo na idadi ya wanaojitokeza kuandamana imepungua kwa kiasi kikubwa.Wengi wa viongozi hao hawajulikani wanakozuiliwa akiwemo Mursi na maafisa wa usalama wameendeleza kampeini yao ya kuwakamata hata viongozi walio majimboni pia.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/Reuters

Mhariri: Sekione kitojo