1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali za Umoja wa Ulaya zakubaliana kuhusu mgawo wa gesi

26 Julai 2022

Serikali za Umoja wa Ulaya Jumanne zimekubaliana kuhusu mgawo wa gesi asilia wakati wa msimu wa baridi kujilinda dhidi ya upunguzaji wowote zaidi wa gesi na Urusi wakati inapoendeleza vita vyake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4EgI0
Brüssel Albanien und Nord-Mazedonien starten EU | von der Leyen
Picha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

Mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha rasimu ya sheria ya Ulaya inayokusudiwa kupunguza mahitaji ya gesi kwa asilimia 15 kuanzia Agosti hadi Machi. Sheria hiyo mpya inahusisha hatua za hiari za kitaifa za kupunguza matumizi ya gesi na ikiwa

hazitaleta tofauti kubwa katika uokoaji wa gesi hiyo basi zitachochea hatua za lazima katika muungano huo wa wanachama 27.

von der Leyen asifu rasimu ya sheria 

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amepongeza hatua hiyo na kusema katika kwamba Umoja wa Ulaya umechukuwa hatua ya maamuzi ya kukabiliana na tishio la kuvurugwa kikamilifu kwa usambazaji wa gesi na rais wa Urusi Vladmir Putin. Makubaliano hayo ya ngazi ya mawaziri yamefikiwa chini ya wiki moja na yanatokana na pendekezo la Jumatano iliyopita la halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya. Ikiwa makini kudumisha msimamo sawa wa Umoja huo wa Ulaya kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine visivyokuwa na dalili ya kumalizika, halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya imesema mgawo ulioratibiwa utaiwezesha kanda hiyo kwa ujumla kupita katika majira ya baridi iwapo Urusi itasitisha usambazaji wote wa gesi yake.

Tschechien Industrieminster Jozef Sikela
Jozef Sikela - waziri wa viwanda wa Czech,Picha: Katerina Sulova/dpa/CTK/picture alliance

Jozef Sikela, waziri wa viwanda wa Czech, amesema kuwa majira ya baridi yanakuja na hawajui yatakuwa baridi kiasi gani.  Sikela ameongeza kuwa kile wanachofahamu kwa uhakika ni kwamba Putin ataendelea kucheza michezo yake mibaya na kutoa vitisho kupitia usambazaji wa gesi. Siku ya Jumatatu,  kampuni kubwa ya nishati ya Urusi Gazprom ilisema itapunguza usambazaji wa gesi kuelekea Umoja wa Ulaya kupitia bomba la Nord Stream 1 hadi 20% ya uwezo wake na kuongeza wasiwasi kwamba Putin atatumia biashara ya gesi kukabiliana na upinzani wa jumuiya hiyo dhidi ya vita nchini Ukraine.

Huku hayo yakijiri, ikulu ya rais wa Urusi,  imesema Jumatatu kuwa kifaa cha gesi kilichofanyiwa matengenezo katika bomba la Nord Stream 1 linalotumika kusafirisha gesi kuelekea Ulaya, hakijawasili baada ya kufanyiwa matengenezo nchini Canada na kwamba kifaa cha pili pia kimeanza kuonesha kasoro.