Shaka ya kutokea machafuko kati ya Syria na Uturuki imetanda
24 Juni 2011Akinukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, Waziri wa Mambo yanchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema hivi sasa wanafanya majadiliano kuhusu hali hiyo na maafisa wa Uturuki.
Mashahidi wamesema wanajeshi wamekusanyika karibu na mpaka wa Utruriki, jambo ambalo linasababisha shaka kwa serikali ya Uturuki wakati huu ambapo Rais Bashair al-Assad akizidisha matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya maandamano yaliyodumu kwa miezi mitatu sasa.
Uturuki imesema mawaziri wa mambo ya nje wa pande hizo mbili wamefanya mashauriano kuhusu suala hilo kwa njia ya simu na balozi wa Syria nchini Uturuki aliitwa kwenye ofisi za wizara ya mambo ya nje ili kuoneshwa namna ambavyo Uturuki ilivyokuwa na wasiwasi juu ya hali ya mambo inavyoendelea huko upande wa mpakani wa kusini/msahariki.
Mwenyekiti wa Shirika la Misaada ya Kiutu la Uturuki, Tekin Kacukali anasema " Mpaka sasa tumeshajenga kambi, na wakimbizi wapo 11,000 na tumekwisha chukua tahadhari yote ili wapatiwe vituo vyote wanavyovihitaji."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton amesema mwenendo wa Syria unaoripotiwa wa kuuzingira na kuulenga mji wa Khirbat al-joz uliopo umbali wa kilometa 500 kutoka mpaka wa Syria na Uturuki unatoa wasi wasi wa kuzuka awamu mpya ya jaribio la nchi hiyo kuzima maandamano.
Clinton amesema na pamoja na kuongeza zaidi tatizo la wakimbizi bado kuna uwezekano wa kutokea mgogoro zaidi baina ya nchi hizo mbili kutokana na hali ilivyo katika eneo hilo la mpakani.
Kufuatia hali hiyo, Clinton amesema amekwisha fanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu na rais Barack Obama alizungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Tayyip Erdogan.
Kwa ujumla Marekani imesema hairidhishwi na mwenendo wa ukandamizaji unaofanywa na Assad kwa kusema anapoteza uhalali wa kuongoza na kumtaka afanikishe mabadiliko alioahidi au kuondoka kabisa madarakani.
Nao Umoja wa Ulaya umeongeza vikwazo zaidi dhidi ya Syria ambapo hivi sasa vimejumuisha walinzi watatu wa kikosi maalum cha kimapinduzi cha Iran kutokana na tuhuma za kuhushwa na kitendo cha kumsadia Assad kuwakandamiza wananchi wake.
Makundi ya Haki za binadamu yanasema kiasi ya watu 1,300 wameuwawa tangu kuanza kwa maandamano ya kuupinga utawala wa nchi hiyo tangu mwezi machi.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/RTR
Mhariri: Abdul-Rahman