1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Israel laua watu 10 wa familia moja Gaza

13 Agosti 2024

Shambulizi la Israel limewaua watu 10 wa familia moja huko Gaza, kusini mwa wilaya ya Khan Yunis, wakati hali ya wasiwasi ya kuzuka vita kamili katika eneo la Mashariki ya Kati ikiendelea kuongezeka.

https://p.dw.com/p/4jQUd
Majengo yaliyoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel Khan Yunis
Majengo yaliyoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel Khan YunisPicha: Bashar Taleb/AFP

Duru za kitabibu zimeeleza kuwa wanafamilia hao wa familia ya Abu Haya wameuawa katika shambulizi la Israel lililotokea Jumanne huko Abassan, mashariki mwa Khan Yunis. Afisa wa afya kutoka katika hospitali ya Nasser amesema mtoto mmoja mchanga wa kike mwenye miezi mitatu, ndiyo pekee aliyesalimika katika shambulizi hilo.

Waliouawa ni wazazi wawili na watoto wanane. Wafanyakazi wa mashirika ya uokozi, walioshuhudia na duru za kitatibu zimeripoti kutokea kwa mashambulizi mengine zaidi ya anga ya Israel na makombora kwenye maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza Jumanne, mengine yakiwa yamesababisha mauaji.

Hayo yanajiri wakati ambapo Marekani imeonya kuwa Iran inaweza kufanya shambulizi dhidi ya Israel wiki hii, wakati hali ya wasiwasi ya kuzuka vita kamili katika eneo la Mashariki ya Kati ikiendelea kuongezeka.

Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John Kirby
Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John KirbyPicha: Ken Cedeno/UPI/newscom/picture alliance

Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John Kirby amesema wanapaswa kuwa tayari kwa mashambulizi ambayo yanaweza kuwa makubwa. Amesema kwamba Marekani imeshirikishana na Israel tathmini kuwa hatua kama hiyo inaweza kuchukuliwa wiki hii.

''Nataka tu kusisitiza kuwa tunaendelea kufuatilia kwa karibu hali inayoendelea Mashariki ya Kati na bila shaka, kuongezeka kwa mvutano huko. Tunapeleka ujumbe kwamba hatutaki kuona ongezeko lolote la ghasia na mashambulizi yoyote ya Iran na washirika wake,'' alisisitiza Kirby.

Biden azungumza na washirika wake wa Ulaya

Kirby alikuwa akizungumza Jumatatu na waandishi habari, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuzungumza na viongozi wenzake wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia, ambapo walijadiliana kuhusu uwezekano wa kusitishwa mapigano huko Gaza, na njia za kupunguza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati.

Iran kwa upande wake imetupilia mbali wito wa mataifa ya Magharibi wa kuacha vitisho vyake vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh ikisema kuwa wito huo hauna mashiko ya kisiasa na unakinzana na kanuni za sheria za kimataifa.

Raia wakiwa katika mji wa Tel Aviv
Raia wakiwa katika mji wa Tel AvivPicha: Nir Alon/ZUMA Press/picture alliance

Aidha, Iran imesema mazungumzo kuhusu makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza yanayotarajiwa kufanyika wiki hii, ndilo jambo la pekee la msingi litakaloisababishia nchi hiyo kutofanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel. Maafisa wa Iran wanaohusika na masuala ya usalama wamesema Iran pamoja na washirika wake kama Hezbollah watashambulia iwapo mazungumzo ya Gaza hayatopata mwafaka au iwapo Israel itakuwa inasuasua katika suala la upatikanaji wa suluhu.

Al-Qassam warusha roketi mbili Tel Aviv

Wakati huo huo, tawi la kijeshi la Hamas, al-Qassam Brigades siku ya Jumanne limesema limeulenga mji wa Tel Aviv na vitongoji vyake kwa mashambulizi mawili ya roketi chapa M90, baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kuwaua watu 19.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa miripuko ilisikika Tel Aviv, lakini hakuna taarifa za kuwepo majeruhi. Kikosi cha al-Qassam Brigades kimesema katika taarifa yake kwamba mashambulizi hayo ni kujibu uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya raia na kuwahamisha watu wao kwa makusudi.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, vita vya Gaza vilivyochochewa na shambulizi la Hamas Oktoba 7, vimesababisha vifo vya watu wapatao 39,929.

(AFP, DPA, Reuters)