Sherehe zapigwa marufuku Dar es Salaam wakati wa maombolezo
19 Machi 2021Kwa mujibu wa ratiba iliotolewa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jiji hili kuu la kibiashara nchini limepata fursa ya siku mbili ambayo ni Machi 20 ambapo viongozi watapata fursa ya kuaga huku Machi 21 wananchi watatoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao aliekuwa Rais Hayati John Magufuli.
Kufuatia ratiba hiyo mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amepiga marufuku mbele ya waandishi wa habari, kwa wakaazi wa jiji hilo kufanya sherehe ya aina yoyote katika kipindi hiki cha siku ishirini na moja za maombolezo na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuheshimu msiba wa kiongozi huyo.
Akitangaza ratiba ya kuanza kwa shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu Rais Magufuli, amewataka wananchi wote bila kujali itikadi zao kuhudhuria katika tukio hilo na kuwataka viongozi wa taasisi za umma na zile za kibinafsi kuwaruhusu watumishi wao kwenda kutoa heshima zao za mwisho.
Kufuatia marufuku hiyo kumezuka mseto wa mawazo kutoka kwa wananchi wengine wakionesha kutofurahishwa na maamuzi hayo ya mamalaka, kwani wengi waliahirisha sherehe zao za kijamii hadi pale atakapozikwa kiongozi wao na si kipindi cha siku 21 kwani itawaletea hasara kwenye bajeti na mipango yao.
katika hatua nyingine baraza la sanaa nchini nalo limesitisha vibali vya matamasha na burudani kwa muda wa siku kumi na nne, ili kutoa nafasi kwa wananchi kuomboleza kifo cha Rais magufuli.
Rais Magufuli ambae amelitumikia taifa hilo kwa kipindi cha miezi mitano tu tangu alipochaguliwa kuliongoza taifa hilo kwa awamu ya pili na ya mwisho kikatiba, alifariki mnamo machi 17 kutokana na tatizo la mfumo wa umeme kwenye moyo ambalo alidumu nalo kwa zaidi ya miaka kumi.