1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo la Umoja wa Mataifa kwa Urusi laongezeka

1 Machi 2022

Mabalozi wengi kwenye Umoja wa Mataifa wameunga mkono pendekezo linaloishinikiza Urusi kusitisha mashambulizi yake nchini Ukraine. Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao cha dharura na cha nadra cha Baraza Kuu la Umoja huo.

https://p.dw.com/p/47kgN
USA | UN Vollversammlung in New York | Dringlichkeitssitzung | Proteste
Picha: John Minchillo/AP Photo/picture alliance

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litawapa wanachama wake wote nafasi ya kuzungumza kuhusu vita. Zaidi ya mataifa 110 yamesaini kufanya hivyo, na hotuba zitaendelea hii leo. Baraza hilo ambalo haliruhusu kura ya turufu linatarajiwa kupigia kura azimio litakaloratibiwa na wajumbe wa Umoja wa Ulaya wanaoshirikiana na Ukraine baadaye wiki hii.

Muswada wa azimio hilo ulioonwa na shirika la habari la AP unaitaka Urusi kuacha mara moja matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine na kuondoa wanajeshi wake, lakini pia linataka azimio la amani kupitia mazungumzo na makubaliano.

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wameendelea kujadiliana kuhusiana na uvamizi wa Urusi, baada ya mapema leo rais wa Marekani Joe Biden kuzungumza naviongozi wenzake ikiwa ni pamoja na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ili kuangazia ushirikiano zaidi wa namna ya kuijibu Urusi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, waziri mkuu wa Italia Mario Draghi, rais wa Poland Andrzej Duda na rais wa Romania, Klaus Johannis na viongozi waandamizi wa Umoja wa Ulaya na NATO pia ni miongoni mwa waliohudhuria.

USA I Ständige Vertretung der Russischen Föderation in New York
Ubalozi wa Urusi jijini New York. Urusi imelaani hatua ya Marekani kuwatimua maafisa wake kwenye Umoja wa MataifaPicha: Spencer Platt/Getty Images

Marekani yawatimua mabalozi 12 wa UN.

Katika hatua nyingine, Marekani imewatimua maafisa 12 wa ujumbe wa Urusi katika Umoja wa Mataifa kwa madai ya kujihusisha na ujasusi na kuhatarisha usalama wa taifa hilo. Ujumbe wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa umesema wanadiplomasia hao wametumia vibaya haki ya ukaazi nchini humo. Marekani imesema inachukua hatua hiyo baada ya miezi kadhaa ya ufuatiliaji.

Urusi imelaani hatua hiyo na kuuita ni ya uchokozi.

Na huko Uholanzi, mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC amesema jana kwamba wanapanga kuanzisha uchunguzi haraka iwezekanavyo kuhusu uwezekano wa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu nchini Ukraine.

Karim Khan amesema uchunguzi huo utaangazia madai ya uhalifu uliofanyika kabla ya uvamizi wa Urusi na kuongeza kuwa kwa kuangazia hali ya kuongezeka kwa mzozo katika siku za karibuni, atafuatilia pia madai yoyote yatakayokuwa ndani ya mamlaka ya ofisi yake yatakayofanywa na upande wowote na katika eneo lolote la Ukraine.

Schweiz FIFA Hauptquartier in Zürich
Picha: Reuters/A. Wiegmann

FIFA na UEFA sasa yasimamisha Urusi kushiriki michuano yake.

Na katika ulimwengu wa soka, shirikisho la soka ulimwenguni FIFA na la Ulaya, UEFA yameisimamisha Urusi kwenye michuano yake. FIFA imesimamisha timu ya taifa ya Urusi na vilabu kushiriki michuano yake yote, ikiwa ni pamoja na ya kombe la dunia itakayofanyika Qatar. Pamoja na michuano ya FIFA, Urusi pia imezuiwa kushiriki michuano ya shirikisho la soka Ulaya, UEFA hadi taarifa nyingine itakapotolewa.

Huku hayo yakiendelea, kampuni kubwa ya mafuta ya Shell imetangaza nia ya kufunga shughuli zake nchini Urusi. Mtendaji mkuu wa Shell Ben van Beurden amesema wameshtushwa na vifo nchini Ukraine na uvamizi unaotishia usalama wa Ulaya. Kampuni ya mafuta ya BP tayari imesitisha ushirikiano na kampuni ya mafuta ya Rosnet ya Urusi.

Tukisalia Urusi, mamia ya waandamanaji wamekamatwa tena katika maandamano ya kupinga uvamizi huo. Shirika la haki za binaadamu la OVD-info limesema karibu watu 412 walikamatwa jana katika miji mbalimbali,  wengi wao kutokea Moscow na St. Petesburg.

Tangu kuanza kwa maandamano hayo Alhamisi iliyopita, zaidi ya watu 6,440 wamezuiwa vizuizini.

Mashirika: DW/APE/DPAE