Syria na urusi zashtumiwa kwa 'uhalifu wa kivita' Syria
11 Mei 2020Tangu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2019, vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi vimefanya kampeini kali za kijeshi dhidi ya ngome ya mwisho inayoshikiliwa na waasi ya Idlib ambayo imekuwa makazi kwa takriban watu milioni tatu.Hatua ya kusitishwa kwa mapigano imechukuliwa tangu mapema mwezi Machi lakini maelfu ya watu bado hawana makazi na wanategemea zaidi misaada hata baada ya eneo hilo linalodhibitiwa na kundi la kijihadi kujiandaa kwa uwezekano wa kuzuka kwa mripuko wa virusi vya corona.
Shirika hilo la Amnesty limesema kuwa limerekodi mashambulizi 18 katika taasisi za matibabu na shule yaliyofanywa aidha na serikali ya Syria ama Urusi ambayo ni taifa mshirika wake kati ya tarehe 5 mwezi Mei mwaka 2019 na 25 Februari mwaka 2020 karibu na ngome hiyo ya waasi.
Katika ripoti yake, shirika hilo limesema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa mashambulizi hayo yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria na Urusi yalijumuisha ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kwamba ukiukaji huo umefikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Aina ya mashambulizi yaliotekelezwa
Shirika hilo limeendelea kusema kuwa mashambulizi hayo yalijumuisha matatu ya ardhini na mawili ya mapipa ya mabomu yaliyofanywa na vikosi vya serikali ya Syria ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya angani kutoka pande hizo mbili ama moja.
Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa mashambulizi makubwa yalifanywa mwezi Januari na Februari mwaka 2020 wakati wa uvamizi wa hivi karibuni ambao kutoka mwezi Desemba umesababisha vifo vya takriban raia 500 na kuwafanya takriban watu milioni moja kupoteza makazi.
Ripoti hiyo imezingatia mahojiano na watu zaidi ya 70 wanaojumuisha walioshuhudia , waliopoteza makazi, madaktari, walimu, wafanyikazi wa mashirika ya msaada na wale wa Umoja wa Mataifa. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Syria na Urusi haukujibu maswali kuhusu shtuma hizo.
Urusi ni mshirika muhimu wa serikali ya Syria katika mzozo huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka tisa. Ndege za Urusi zilianza kutekeleza mashambulizi katika ngome za waasi mnamo mwezi Septemba mwaka 2015. Kwa usaidizi wa Urusi, serikali ya rais Bashar al- Assad imeweza kukomboa maeneo muhimu.