Shirika la Japan lashinda Tuzo ya Amani ya Nobel
11 Oktoba 2024Tuzo hiyo iliyotangazwa muda mfupi uliopita huko Oslo, imetunukiwa shirika la Nihon Hidankyo, linalojulikana pia kama Hibakusha.
Kamati ya tuzo ya Nobel ya Norway imesema tuzo ya amani ya mwaka huu imetolewa kwa shirika hilo la Hibakusha kutokana na juhudi zake za kuifanya dunia kuondokana na silaha za nyuklia pamoja na kuonesha kupitia ushahidi wa walionusurika, kwamba silaha za nyulika hazipaswi kutumiwa tena.
Kiongozi wa shirika hilo, Toshiyuki Mimaki akizungumza baada ya ushindi akiwa huko Hiroshima, amesema ushindi huo utakuwa nguvu kubwa ya kutowa mwito kwa dunia kuzipiga marufuku silaha za nyuklia.
Sherehe za kukabidhi tuzo hiyo yenye thamani ya dola milioni 1 itafanyika tarehe 10 Desemba mjini Oslo, siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa tuzo hizo Alfred Nobel raia wa Sweden.