Shirika la OPCW kupokea tuzo yake rasmi siku ya Jumanne
8 Desemba 2013Katika kulitangaza shirika hilo la OPCW kama mshindi wa tuzo ya Nobel mwaka wa 2013 mnamo Oktoba 11, mwenyekiti wa Kamati ya Norway ya Nobel Thorbjoern Jagland, aliangazia jukumu la shirika hilo kuwa mfano wa mafanikio ya kuangamiza silaha duniani.
Shirika hilo lilipewa rasmi zawadi hiyo kwa juhudi zake duniani kote, lakini tuzo hiyo ilitolewa wakati macho ya dunia nzima yakiliangalia taifa la Syria baada ya shambulizi la gesi ya sumu lililosababisha mauaji ya mamia ya watu nje kidogo ya mji wa Damascus mnamo Agosti 21.
Siku ya Jumanne wiki hii mkurugenzi wa OPCW Ahmet Uzumcu atakabidhiwa tuzo hiyo wiki kadhaa kabla ya zoezi la kuharibu hazina ya silaha za sumu za Syria kuanza.
Kulingana na makubaliano kati ya Marekani na Urusi yaliyozuia serikali ya Bashar al Assad kuingiliwa Kijeshi na Marekani, Syria inapaswa kuharibu silaha hizo za sumu zinazofikia tani 1,290 kabla ya katikati ya mwaka ujao.
Changamoto kwa shirika la OPCW
Licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana na wafanyakazi wa shirika hilo walioko Syria kuanzia Mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, bado kuna changamoto kubwa alisema Sigrid Kaag mnamo Disemba 2.
Kaag alisema hali ya usalama katika taifa hilo ambalo watu zaidi ya 126,000 wameuwawa miezi 33 tangu kuanza kwa machafuko nchini humo, ni moja ya mambo yanayotoa changamoto kubwa kwa shirika hilo kutekeleza kazi yake ipasavyo.
Hata hivyo tayari shirika la OPCW linaonekana na wengi kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. kwa sasa inawanachama mataifa 190 ikiwemo karibu mataifa yote ya viwanda na zaidi ya asilimia 98 ya idadi ya watu duniani.
Israel na Myanmar wametia saini maagano ya kuangamiza silaha za sumu lakini bado hawajaidhinisha, wakati Angola,Misri, Korea Kaskazini na Sudan Kusini wameshindwa kutekeleza hilo.
Msemaji wa OPCW Michael Luhan amesema kwa vyovyote vile tuzo hiyo ya amani ya Nobel ambayo imempoteza mmoja wa waliopokea tuzo hiyo Nelson Mandela tayari imeinua hadhi ya shirika hilo la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu.
Tuzo ya amani ya Nobel inajumuisha medali ya dhahabu, cheti, na kitita cha dola milioni 1.2 au euro 898,000.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo