Shirikisho la DFB lawasiliana na wakala wa Nagelsmann
15 Septemba 2023Gazeti la Bild la hapa Ujerumani limeripoti Alhamisi (14.09.2023) kwamba shirikisho la kandanda la Ujerumani, DFB, limefanya mawasiliano ya kwanza na wakala wa kocha Julian Nagelsmann, huku likiwa chini ya shinikizo la kumtafua kocha mpya kabla mashindano ya kombe la EURO 2024 yatakayofanyika nyumbani. Kocha wa zamani Hansi Flick alitimuliwa Jumapili iliyopita kufuatia kichapo cha goli 4-1 kutoka kwa Japan katika mechi ya kirafiki na kwa kupata ushindi mara nne tu katika jumla ya mechi 17 zilizopita.
Gazeti la Bild limesema mkurugenzi wa shirikisho la soka la Ujerumani, Rudi Voller, ambaye aliisimamia timu ya taifa wakati ilipoishinda Ufaransa 2-1 katika mechi ya kirafiki siku ya Jumanne, amewasiliana na wakala wa Nagelsmann, Volker Struth.
Nagelsmann alitimuliwa na klabu ya Bayern Munich mnamo mwezi Machi mwaka huu, lakini bado ana mkataba na mabingwa hao wa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga hadi 2026. Hata hivyo, gazeti la Bild liliripoti mapema wiki hii kwamba Bayern itafuta gharama ya uhamisho iwapo Nagelsmann ataafikiana na shirikisho la DFB.
Kwa mabadilishano shirikisho hilo litalipa asilimia 100 ya mshahara wa Nagelsmann. Bayern pia haitomlipa Nagelsmann marupurupu kwa kumuachisha kazi. Rais wa heshima wa klabu ya Bayern Uli Hoeneß pia amesema klabu hiyo haitayakwamisha mazungumzo kati ya Nagelsmann na shirikisho la DFB.
Majina kadhaa yanatajwa
Kocha wa mpito Rudi Völler amesisitiza hatapatikana kwa muda mrefu kuiongoza timu ya taifa ya Ujerumani na yeye pamoja na rais wa shirikisho la DFB Bernd Neuendorf wamekataa kutaja majina ya makocha wanaopigiwa upatu kuchukua nafasi iliyowachwa na kocha Hansi Flick.
Kocha wa Liverpool Jürgen Klopp anabaki kuwa na nafasi kubwa, huku Matthias Sammer akisemekana hatapatikana kutokana na matatizo ya kiafya aliyoyapata miaka michache iliyopita. Ralf Rangnick amesema ataendelea kuwa kocha wa Austria na kocha wa zamani wa timu ya Ujerumani ya vijana wa umri wa chini ya miaka 21, Stefan Kunz, ni kocha wa Uturuki. Kocha mkongwe, Felix Magath, na kocha raia wa Austria Oliver Glasner pia wametajwa.
Mechi zijazo za Ujerumani zitachezwa Oktoba 14 huko Hartford dhidi ya Marekani na siku tatu baadaye huko Philadelphia dhidi ya Mexico. Shirikisho la DFB limesema lina matumaini kocha mpya atapatikana kabla mechi hizo.
Wachezaji wanawake wasitisha mgomo Uhispania
Tukiacha na hayo huko nchini Uhispania, wachezaji wa soka wanawake katika ligi wamesitisha mgomo wao baada ya maafikiano ya kuongezwa mshahara wa kima cha chini anaoweza kulipwa mchezaji. Hayo yamesemwa na viongozi wa ligi na vyama vya wafanyakazi. Mechi za kwanza za msimu hazikuchezwa wikendi iliyopita kutokana na mgomo huo, lakini mechi za mzunguko wa pili sasa zitaendelea kama ilivyopangwa.
Soma pia: Rubiales atafikishwa mahakamani
Mshahara wa chini kabisa katika ligi ya wanawake Uhispania sasa ni euro 16,000 ikilinganishwa na 182,000 katika ligi ya wanaume. Makubaliano mapya yataongeza kima cha chini cha mshahara katika ligi ya wanawake hadi euro 21,000 msimu huu, huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka hadi 23,500 kufikia mwaka 2025. Kinaweza hata kuongezeka zaidi ya hapo kutegemea na mapato.
Msimu uliopita wachezaji 80 kati ya 334, walipokea chini ya euro 20,000 kwa mwaka, huku kiwango cha wastani cha mshahara kikiwa takriban euro 40,000 kwa mujibu wa viongozi wa ligi.
Mgomo huo, ambao ulitangazwa wiki iliyopita na wachezaji, ulisadifiana na kashfa iliyomkabili rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales alipombusu mchezaji wa timu ya taifa mdomoni bila ridhaa yake wakati wa shughuli za utoaji tuzo baada ya fainali ya mashindano ya kombe la dunia. Rubiales alijiuzulu siku ya Jumapili.
(dpa,ap)