1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha za sumu zilitumika Syria

Caro Robi6 Mei 2013

Waasi nchini Syria walitumia sumu ya Sarin inayoathiri neva za ubongo katika vita vya Syria.Hayo ni kulingana na mchunguzi wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Carla del Ponte

https://p.dw.com/p/18SmM
waathiriwa wa sumu Syria
waathiriwa wa sumu SyriaPicha: Reuters

Aliyekuwa Mwendesha mkuu wa mashtaka ya uhalifu Carla del Ponte katika mahojianao na kituo kimoja cha redio cha Uswisi amesema kulingana na ushahidi waliokusanya,waasi wa Syria walitumia silaha za kemikali kwa kutumia sumu hatari ya sarin.

del Ponte amesema bado wataendelea kufanya uchunguzi wa kina kuthibitisha hali hiyo kupitia mashahidi wapya na kwamba tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa bado haijakamalisha uchunguzi wake.

Tume hiyo ambayo inapaswa kuwasilisha uchunguzi wake kwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao chake kijacho mwezi Juni huenda ikapata ushahidi kuwa utawala wa Syria pia ulitumia sumu hiyo.

mchunguzi wa Umoja wa Mataifa Carla Del Ponte
mchunguzi wa Umoja wa Mataifa Carla Del PontePicha: AP

Sumu ilitumika katika vita vya Syria

Sarin ni sumu kali inayoathiri neva za ubongo ambayo ilitengezewa na wanasayansi wa kinazi katika miaka ya 1930.Mwanzoni ilitengezwa kutumika kama dawa ya kukabiliana na wadudu lakini ilitumika katika shambulio dhidi ya kijiji cha wakurdi cha Halabja nchini Iraq mwaka 1988 na pia kundi moja la itikadi kali la Japan lilitumia mara mbili katika miaka ya 90.

Huku hayo yakijiri,maafisa wa afya nchini Uturuki wanachukua vipimo vya damu vya wakimbizi wa Syria waliokimbilia nchini humo wakiwa na majeraha ili kubaini kama wameathirika na kemikali hiyo ya Sarin.

Mataifa ya magharibi yameingiwa na wasiwasi kuhusu matumizi ya silaha za kemikali kati ya utawala wa Rais Bashar al Assad na waasi wanaotaka kumng'oa madarakani.

Wakati huo huo Israel inajaribu kumshawishi Rais wa Syria kuwa mashambulio yao ya angani mwishoni mwa juma mjini Damascus hayakulenga kumhujumu.

Ndege ya kivita ya Israel
Ndege ya kivita ya IsraelPicha: Getty Images

Israel haitarusu silaha zifikie Hezbollah

Maafisa wamesema Israel inasita kuegemea upande wowote wa vita hivyo vya Syria kwa kuhofia kuwa hatua hiyo itayapa nguvu makundi ya kiislamu yenye itikadi kali ambayo ni mahasimu wa Israel zaidi ya uhasama na familia ya Assad ambao umekuwepo tangu jadi.

Israel imeonya mara kwa mara kuwa haitaruhusu kundi la wanamgambo la Hezbolla washirika wa Assad kupewa silaha za kisasa zenye uwezo mkubwa.Israel ilishambulia shehena ya silaha siku ya Jumamosi zinazoaminika zilikuwa zikipelekwa kwa kundi hilo lenye makao yake nchini Lebanon.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria limesema mashambulio hayo ya Israel ya jana karibu na mji mkuu Damascus,yamewauwa karibu wanajeshi 15 na wengine wengi hatma yao haijulikani kwani maeneo matatu yaliyolengwa kwenye mashambulio hayo huwa yana karibu wanajeshi 150.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters.

Mhariri: Saumu Yusuf.