Simu ya mwisho ya Obama kwa Merkel
20 Januari 2017Katika taarifa yake msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa ulimwengu katika mazungumzo yao kwa njia ya simu.
Sehemu ya taarifa hiyo inasema " Rais na Kansela wamekubaliana kuwa ushirikiano wa karibu baina ya Washington na Berlin na kati ya Marekani na Ulaya ni muhimu katika kuhakikisha mahusiano ya Atlantic, taratibu za amani ya dunia na utetezi wa misingi ambayo hadi sasa imesaidia kusukuma maendeleo ya binadamu baina ya mataifa hayo na duniani kote".
Obama amemshukuru Merkel kwa uongozi wake thabiti na kwamba baada ya kufanya kazi pamoja kwa miaka minane, ilikuwa inafaa simu yake ya mwisho kuzungumza na Merkel.
Mke wa Obama Michelle, aliungana na mume wake katika mazungumzo hayo ambayo pia yalimhusisha mume wa Bi Merkel.
Obama aliwahi kumuelezea Merkel kama mmoja wa mshirika wake wa karibu wa kimataifa katika kipindi cha miaka minane, ingawa mahusiano yao hayakuwa ya kuridhisha. Urafiki wao ulitikisika baada ya nyaraka zilizovuja mwezi Oktoba 2013 na kuonyesha namna Marekani ilivyowapeleleza viongozi washirika wake wa kigeni akiwemo Merkel, ambapo mazungumzo ya simu ya Kansela Merkel yalikuwa yakifuatiliwa.
Hata hivyo kiwango cha ukaribu wao kimekuwa dhahiri baada ya Obama hivi karibuni kumuunga mkono Merkel katika mzozo wa wakimbizi wa barani Ulaya na kumsifu kuwa alikuwa sahihi katika kuandika historia.
Merkel pia alionekana kutokuwa na kinyongo na kuyaacha ya zamani yapite ambapo mwezi Aprili alinukuliwa akisema kwake mustakabali wa baadae na rais huyo ulikuwa wa umuhimu mkubwa kuliko yalopita.
Mtazamo chanya wa Obama kwa kiongozi wa Ujerumani hata hivyo unaonekana kukinzana na matamshi yaliyotolewa na rais anayesubiri kuapishwa Donald Trump, katika mahojiano yake na magazeti mawili ya barani Ulaya siku ya Jumapili, Trump alimshambulia na kumkosoa Merkel na kumuiita kuwa ni "janga" kwa uamuzi wake wa kufungua mipaka ya Ujerumani kwa maelfu ya wakimbizi na wahamiaji.
Trump aliweka wazi pia kwamba Jumuiya ya kujihami ya NATO ni ya kizamani akisema nchi nyingi zitaondoka Umoja wa Ulaya kama ilivyofanya Uingereza.
Matamshi ya kiongozi huyo yalikemewa na pande zote mbili. Wasaidizi wa Trump tangu wakati huo wamejaribu kusahihisha matamshi hayo wakisisitiza kwamba Trump anahitaji mahusiano mazuri na kiongozi wa Ujerumani.
Viongozi wa Ulaya wamekuwa na wasiwasi juu ya rais huyo ajaye asiyetabirika na namna anavyoiunga mkono Urusi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DW/AFP/DPA
Mhariri: Saumu Yusuf