Soko la kale laungua moto Aleppo
30 Septemba 2012Vuguvugu la mageuzi lililogeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vinaendelea hivi sasa nchini Syria vimesababisha watu 30,000 kupoteza maisha yao, kwa mujibu wa makundi ya wanaharakati nchini Syria kama kundi linaloangalia haki za binadamu nchini humo lenye makao yake makuu mjini London.
Lakini mbali na gharama ya upotevu wa maisha ya watu , lakini nyingi ya hazina za kihistoria pia zimeharibiwa katika mzozo huo uliodumu sasa miezi 18, ambao umeyaacha baadhi ya maeneo ya miji kuwa magofu.
Mashambulio mapya mjini Aleppo
Wapiganaji wanaopigana kumwondoa madarakani rais Bashar al-Assad wametangaza kuwa wamefanya shambulio jipya dhidi ya mji wa Aleppo, mji wa kibiashara wa Syria wenye wakaazi wapatao milioni 2.5, siku ya Alhamis, lakini hakuna upande unaoonekana kupata ushindi.
Mjini Aleppo , wanaharakati wakizungumza kupitia mtandao wa Skype wamesema wanajeshi wa serikali waliokaa katika maeneo maalum wakiwalenga watu shabaha, wanafanya hali kuwa ngumu kwa wao kukaribia eneo la Souk al-Madina, soko la kale lenye njia nyembamba lililoko katika mji mkongwe, ikiwa ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii.
Soko laungua
Video vizilizowekwa katika tovuti ya You Tube katika mtandao wa internet , zinaonesha wingu kubwa jeusi likitanda katika anga la mji huo.
Wanaharakati wamesema kuwa moto umezuka kutokana na mashambulio ya makombora na risasi siku ya Ijumaa na wanakadiria kuwa kati ya maduka 700 hadi 1,000 yameharibiwa hadi sasa. Maelezo hayo ni vigumu hata hivyo kuweza kuthibitishwa, kwasababu serikali inazuwia vyombo vya habari vya kimataifa.
Mji mkongwe uliopo mjini Aleppo ni moja kati ya maeneo yaliyotengwa na shirika la umoja wa mataifa ya sayansi na utamaduni UNESCO, kuwa turathi ya dunia, ambapo hivi sasa umo katika hatari kutokana na mapigano hayo.
Maeneo mengine hatarini
UNESCO inaamini kuwa maeneo matano kati ya sita ya turathi nchini Syria , ambayo pia ni pamoja na mji wa kale uliopo jangwani wa Palmyra na sehemu za mji mkongwe mjini Damascus yameathirika.
Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu mjini London , ambalo linamtandao wake wa wanaharakati nchini Syria , limesema kuwa majeshi ya Assad na waasi wanalaumiana kila mmoja kwa kuzusha moto huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani