Sri Lanka hatimae yapewa fedha na IMF za kuinusuru kiuchumi
21 Machi 2023Rais wa nchi hiyo Ranil Wickremesinghe : '' Sri Lanka sio tena taifa muflisi. Kwahivyo tunaweza kuanza tena kufanya miamala ya kawaida. Wakati hali yetu ya ubadilishanaji fedha za kigeni ikiimarika tutaondowa hatua kwa hatua vikwazo vya uagizaji nje. Bidhaa muhimu, dawa na vitu vingine vinavyohitajika katika sekta ya utalii vitakuwa katika awamu ya kwanza.''
Sri-Lanka itapokea fungu la kwanza la dola milioni 330 katika kipindi cha siku mbili zijazo kwa mujibu wa IMF ambazo zitaiwezesha nchi hiyo kuanza kudhibiti viwango vyake vya madeni. Wafuasi wa rais Wickremesinghe wamesherehekea uamuzi huo wa IMF kwa kuwasha fashfash katika mitaa ya mji mkuu Colombo.
Soma pia: Sri Lanka inawezaje kujikwamua kwenye mzozo wake wa kifedha?
Nchi hiyo iliingia kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi kufuatia usimamizi mbaya wa kiuchumi. Kadhalika janga la virusi vya Corona lilizidisha hali kuwa mbaya zaidi na kuitumbukiza nchi hiyo katika ukosefu mkubwa wa sarafu ya dola uliosababisha matatizo katika uagizaji bidhaa muhimu nchini humo.