Steinmeier: Sote tunamani ulimwengu wa amani zaidi
25 Desemba 2023Katika hotuba yake ya kila mwaka ya Krismasi aliyoitoa usiku wa kuamkia leo, Steinmeier amesema, mwaka huu, kwa hakika ulimwengu umedhihirisha upande wake wa giza.
Ameongeza kuwa vita vya uchokozi vya Urusi dhidi ya Ukraine sasa vinaingia katika msimu wa pili wa majira ya baridi kali.
Steinmeier amezungumzia pia yanayojiri Mashariki ya Kati ukiwemo ule aliouita "ukatili wa Hamas" na yanayotokea kwa wahanga wa vita vya eneo hilo.
Soma pia: Steinmeier awaonya wananchi kutoipa kisogo demokrasia
Licha ya changamoto hizo, Steinmeier amesisitiza umuhimu wa matumaini na haja ya kuukaribia mwaka mpya kwa ujasiri.
Rais huyo wa Ujerumani amesisitiza umuhimu wa kudumisha demokrasia imara, akisema hilo linaweza kutokea tu ikiwa watu watashirikishwa na ikiwa watajitahidi kuhakikisha kwamba kile ambacho bado hakijawa kizuri leo, kinakuwa bora kesho.