1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Strauss-Kahn ajiuzulu ukuu wa IMF

19 Mei 2011

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Dominique Strauss-Kahn, amejiuzulu wadhifa huo wakati akiendelea kubakia rumande kutokana na tuhuma za kujaribu kumbaka mfanyakazi wa kike wa hoteli moja, New York.

https://p.dw.com/p/11JYS
Dominique Strauss-Kahn
Dominique Strauss-KahnPicha: dapd

Taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa Strauss-Kahn imetolewa wakati tayari juhudi za kumtafuta mrithi wake zimeshaanza. Mkuu huyo wa IMF yuko rumande nchini Marekani tokea Jumapili, akisubiri hatima ya kesi yake ya jaribio la kubaka.

Bila ya shaka, Strauss-Kahn ameamua kuondoka kwenye wadhifa wake kufuatia masaibu haya, lakini pia kutokana na shinikizo kutoka kwa watu mashuhuri.

Mapema Jumanne iliyopita, Waziri wa Fedha wa Marekani, Timothy Geithner, alilitaka shirika la IMF kutafuta mtu mwengine kuchukuwa nafasi ya Strauss-Kahn, akisema kwamba kwa sasa Strauss-Kahn hayupo katika hali ya kuweza kuiongoza taasisi hiyo kubwa kabisa la kifedha duniani.

Hata hivyo, hatua hii ya Strauss-Kahn kujiuzulu haikuwashangaza watu tena, japokuwa imefuatiliwa kwa makini kwenye taasisi nyengine za fedha za kimataifa na duniani kote kwa jumla. Katika barua ya kujizulu kwake, mwanasiasa na mchumi huyu wa Kifaransa ameeleza masikitiko makubwa aliyonayo.

Mahakama kuamua dhamana ya Strauss-Kahn

Dominique Strauss-Kahn akiwa mahakamani mjini New York
Dominique Strauss-Kahn akiwa mahakamani mjini New YorkPicha: dapd

Wakati huo huo, leo hii mahakama ya jimbo la New York itaamua iwapo itampa mtuhumiwa huyo wa ubakaji dhamana na hivyo kutoka kwenye jela ya kisiwa cha Rikers.

Katika maombi aliyoyawaslisha mahakamani hapo, wakili wake amejenga hoja kwamba mteja wake yupo tayari kutoa dhamana ya kiasi cha dola milioni moja za Kimarekani.

Wakili huyo amearifu kwamba mteja wake pia yupo tayari kuwamo katika kizuizi cha nyumbani, katika makaazi ya binti yake anayeishi jijini New York. Strauss-Kahn atavalishwa kifaa maalum ili kufuatilia nyendo zake.

Hadi sasa mtu wa kuuchukua wadhifa wa mkurugenzi wa shirika la IMF hajapatikana, japo majina kadhaa yameshatajwa, ikiwa ni pamoja na la Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde.

Na habari kutoka Berlin zinasema wizara ya fedha ya Ujerumani inaamini kwamba atakayemfuatia Strauss-Kahn atatokea Ulaya, na kwamba nchi zinazoinukia kiuchumi zifuatie baadaye. Msemaji wa wizara hiyo alitoa kauli hiyo kufuatia kujiuzulu kwa Strauss-Kahn, akisisitiza aliyoyasema Kansela Angela Merkel mapema wiki hii.

Mwandishi: Klaus Kastan/ARD/ZDF
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi