1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaadhimisha miaka mitatu ya Uhuru

Admin.WagnerD9 Julai 2014

Sudan Kusini leo inaadhimisha miaka mitatu ya uhuru,huku Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewahimiza viongozi wa Sudan Kusini kuumaliza mzozo unaoendelea, ambao amesema umechochewa na wao wenyewe

https://p.dw.com/p/1CYdG
Picha: Ashraf Shalzy/AFP/Getty Images

Katibu huyo mkuu wa umoja wa Mataifa amesema viongozi wa Sudan Kusini ndiyo waliosababisha mzozo unaoendelea hivi sasa katika taifa hilo changa duniani na ni wajibu wao kuumaliza kwani wana nguvu za kufanya hivyo.

Ban Ki-moon ameonya kuwa maelfu ya watu nchini humo huenda wakakabiliwa na kitisho cha uhaba mkubwa wa chakula katika kipindi cha miezi michache ijayo iwapo viongozi wao hawatashirikiana,hawataweka silaha chini na kurejea mara moja katika meza ya mazungumzo.

Maelfu wameuawa,mamilioni bila makaazi

Maelfu ya watu wameuawa nchini Sudan Kusini na wengine kiasi ya milioni moja na laki tatu wamelazimika kuyatoroka makaazi yao tangu yalipozuka mapigano mwezi Desemba mwaka jana kati ya wanajeshi wa serikali ya Rais Salva Kiir na wapiganaji watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar.

Raia wa Sudan kusini kambini wakipokea misaada ya chakula
Raia wa Sudan kusini kambini wakipokea misaada ya chakulaPicha: UNMISS/JC McIlwaine

Leo ni mwaka wa tatu tangu Sudan Kusini kutangazwa kuwa taifa huru baada ya kujitenga na Sudan.Lakini Ban amesema matumaini makubwa waliyokuwa nayo raia wa Sudan Kusini ya maisha bora ya siku za usoni baada ya kujipatia uhuru yalivunjwa baada ya viongozi wao kuchochea ghasia za kikabila kati ya makabila ya Dinka na Nuer.

Mazungumzo ya amani mjini Addis ababa hadi sasa yamekwama.

Hivi karibuni baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilibadilisha mamlaka ya kikosi cha kulinda amani cha kijeshi cha umoja huo nchini Sudan Kusini kutoka kuwa cha kusaidia shughuli za maendeleo na sasa kuwa sasa na mamlaka ya kuwalinda raia.

Ban Ki Moon awashutumu viongozi

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa amesema umoja huo utaendelea kusimama na watu wa Sudan Kusini na kuendelea kufanya kila juhudi kuwapa ulinzi na misaada ya kibinadamu kwani ni haki zao za kimsingi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture alliance/AA

Katika kuadhimisha siku ya uhuru leo hata hivyo,Barabara za mji mkuu Juba zimewekwa mabango yanayotangaza umoja wa taifa hilo huku rais Salva Kiir akitarajiwa kulihutubia taifa katika sherehe zitakazoandamana na gwaride la kijeshi.

Usalama umeimarishwa kote mjini humo kabla ya sherehe rasmi huku wengi wa raia wakisema hawaoni la kusherehekea miaka mitatu baadaye baada ya kujitenga kutoka Sudan kwa mbwembwe na matumaini makubwa.

Shirika la kimataifa la kutoa misaada la Oxfam limeutaja mzozo wa Sudan Kusini kuwa mbaya zaidi barani Afrika huku kiasi ya watu milioni nne wakikumbwa na uhaba mkubwa wa njaa na misaada imeweza tu kuwafikia nusu ya idadi ya wanaohitaji misaada kwa dharura.Kiasi ya watoto elfu hamsini wanahofiwa huenda wakapoteza maisha yao kutokana na utapia mlo iwapo misaada ya dharura haitawafikia kwa haraka.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman