Sudan Kusini yawataka wakimbizi kurejea nyumbani
23 Februari 2023Wito huo wa Rais Salva Kiir alioutoa jana Jumatano ulikuja wakati nchi hiyo ikijiandaa kufanya uchaguzi wake wa kwanza tangu kupata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011.
Uchaguzi uliocheleweshwa wa Sudan Kusini unatazamiwa kufanyika Desemba 2024. Sudan Kusini bado inaendelea kufufuka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano, vilivyozuka mwishoni mwa 2013, na kuua mamia ya maelfu ya watu na kumalizika kwa makubaliano ya amani mwaka 2018.
Kwa muda, raia wa Sudan Kusini waliokimbia waliunda kundi kubwa zaidi la wakimbizi duniani katika nchi jirani ya Uganda. Rais amewahakikishia watu wanaorejea nchini usalama wao, na kutoa wito kwa washirika wa kimataifa kuiunga mkono serikali katika kuwashirikisha tena kwenye jamii.
Mkutano wa rais Kiir umefanyika wiki mbili baada ya Papa Francis aliyezuru taifa hilo, kukutana na raia wa Sudan Kusini waliokimbia makazi yao katika mji mkuu, Juba, na kuomba amani ya kudumu.