Syria kuwasilisha mpango wa silaha za sumu
24 Oktoba 2013Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali limesema hatua hiyo ya serikali ya Syria kukabidhi mpango wa silaha zake za kemikali ni sehemu ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi yaliyoepusha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria ambayo yanataka silaha zote za kemikali na viwanda vya kutengeneza silaha hizo viteketezwe ifikapo katikati ya mwaka wa 2014.
Utawala wa rais Assad tayari umekabidhi taarifa kuhusi kiwango cha silaha hizo pamoja na viwanda, na kundi la pamoja la watalaamu wa Umoja wa Mataifa na Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali limekuwa nchini Syria tangu mapema mwezi huu wakizikagua na kuziangamiza. Msemaji wa shirika hilo Michael Luhan amesema tayari wamekagua maeneo 18 kati ya 23 na kuharibu silaha hizo pamoja na vifaa vyote vya kuzitengeneza.
Lakini uwezekano wa kufanyika mkutano wa amani, ambao Umoja wa Mataifa unajaribu kuandaa kwenda sambamba na shughuli ya uteketezaji wa silaha hizo, unaonekana kukwama baada ya viongozi wa ngazi ya juu wa upinzani kukaidi juhudi za nchi za Kiarabu na za Magharibi kuwashawishi kuhudhuria.
Utawala wa Assad kupitia wizara ya mambo ya nchi za nje pia ulijibu kwa ukali hapo jana kuwa hakuna kundi lolote la kigeni litakalohusika katika kuamua uongozi wa nchi hiyo. Taarifa hiyo ilisema serikali iko tayari kuhudhuria mkutano huo unaopangwa wa Geneva ili “kujaribu iwezavyo kuhakikishia unafanikiwa bila masharti yoyote ya kabla au uingiliaji kati wa kigeni”. Upinzani unatarajiwa kukutana mapema mwezi ujao ili kukamilisha msimamo wao kuhusiana na mazungumzo hayo ya Geneva.
Kwingineko Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria limesema serikali ya Rais Bashar al-Assad imewaachia huru wanawake 61 katika kipindi cha siku mbili zilizopita. Hapajakuwa na taarifa yoyote kutoka upande wa serikali, wala maelezo kuwahusu wanawake hao au mahali waliko kwa sasa.
Kuwachiwa kwao ni sehemu ya mpango uliofikiwa wiki iliyopita wa kubadilishana wafungwa uliosimamiwa na Qatar na Mamlaka ya Palestina ambao uliwafanya waasi wa Syria kuwaachilia huru Walebanon tisa wa madhehebu ya Shia, wakati nao wapiganaji wa Lebanom wakiwaachilia huru marubani wawili wa Kituruki.
Sehemu ya tatu ya mpango huo iliitaka serikali ya Syria kuwaachia huru idadi kadhaa ya wanawake wafungwa ili kutimiza masharti ya waasi. Mjini Damascus, nishati ya umeme inarejea taratibu katika maeneo mbali mbali, baada ya mji huo mkuu kutumbukia gizani hapo jana kufuatia shambulizi la waasi kwenye bomba la mafuta.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba