1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria mapambano zaidi

MjahidA9 Machi 2012

Wanaharakati wa upinzani nchini Syria wamesema vikosi vya serikali nchini humo vimewauwa takriban raia 21 katika mapambano ya kusimamisha maandamano dhidi ya rais Bashar Al Assad.

https://p.dw.com/p/14ISm
Vifaru vya kijeshi nchini Syria
Vifaru vya kijeshi nchini SyriaPicha: AP

Mauaji haya yametokea wakati ambapo, mjumbe maalum wa umoja wa mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu Koffi Annan akijitayarisha kutembelea nchi hiyo.

Vifaru vya kijeshi vilionekana katika wilaya ya Karm al-Zeitoun na wilaya nyengine za upinzani mjini Homs, vikishambulia na kusababisha vifo vya watu wanane. Vifo vengine 12 viliripotiwa mjini Damascus na na katika mkoa wa Hama, Idlib na Aleppo. Karam Abu Rabea, mkaazi katika wilaya ya Karm al-Zeitoun, amesema vifaru vya kijeshi takriban 30 viliingia wilayani humo na kutumia mabomu yaliolenga nyumba za watu.

Maandamano nchini Syria yamekuwa yakifanyika kila siku ya Ijumaa baada ya Sala ya waislamu, tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano la kumshinikiza Rais Assad aondoke madarakani. Hii imekuwa ikifanyika licha ya jeshi la Syria na waasi waliowatiifu kwa serikali ya Bashar kujaribu kudhibiti maandamano hayo.

Mkuu wa misaada ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos
Aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi AnnanPicha: dapd

Mapigano yaliokithiri kwa muda mrefu sasa nchini Syria huenda yakaelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Annan kuanzisha misheni yake Damascus

Hata hivyo Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya nchi za kiarabu anayeshughulikia mzozo wa Syria Koffi Annan, anatarajiwa kwenda mjini Damascus jumamosi hii kuanza misheni yake ya kutafuta amani nchini Syria. Annan ametaka kufanyike mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa.

Aidha Upinzani umesema kwa sasa hakuna nafasi yoyote ya mazungumzo kutokana na vikosi vya Assad kuendelea kuwaangamiza. Vuta ni kuvute miongoni mwa mataifa yalio na nguvu duniani imepiga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutatua mzozo wa Syria, huku China na Urusi ikipinga hatua yoyote itakayofanya Syria kuingiliwa kama ilivyoingiliwa Libya.

Kwa upande wake China imekaribisha misheni ya aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan ya kujaribu kuleta amani nchini Syria. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China Liu Weimin amesema wanatumai Annan atatumia hekima na ujuzi wake kuona kwamba pande zote zinaunga mkono juhudi za kupatikana amani nchini humo.

Valerie Amos
Mkuu wa misaada ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie AmosPicha: AP

China ambayo imepeleka wajumbe wake nchini Syria wiki hii, leo imesema itamtuma naibu waziri wake wa mambo ya kigeni mashariki ya kati na Ufaransa kuzungumzia mzozo wa Syria.

Mkuu wa misaada ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos alitembelea kambi ya wakimbizi ya wasyria nchini Uturuki baada ya kutembea mjini Homs na kuona athari ya ghasia huko.

Umoja wa Mataifa awali ulikadiria watu 7, 500 wameuwawa tangu kuanza kwa ghasia nchini Syria takriban mwaka mmoja uliopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/ RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul- Rahman