Syria yasimamishwa uanachama OIC
15 Agosti 2012Mfalme wa Saudi Arabia Abdullah ameufungua mkutano huo wa jumuiya ya nchi za kiislamu, akikaa karibu na rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, kama ishara ya maridhiano baina ya nchi hizo mbili za kiislamu ambazo zina maoni tofauti juu ya masuala mengi.
Mkutano huo ulitanguliwa na mwingine wa ngazi ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje, ambao ulipitisha jana uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Syria ndani ya jumuiya ya ushirikiano wa nchi za kiislamu, kutokana na ukandamizaji unaofanywa na serikali ya rais Bashar al-Assad dhidi ya upinzani ambao umedumu kwa muda wa miezi 17. Nchi zote wanachama, isipokuwa Iran na Algeria, zilikubaliana na uamuzi huo. Jumuiya hiyo inazo nchi wanachama 57, zenye wakazi wapatao bilioni 1.5.
Assad atakiwa kusimamisha ghasia ''mara moja''
Rasimu ya tangazo la mkutano huo ilisema Syria inapaswa kusimamishwa uanachama kwa sababu imeamua kuendeleza matumizi ya nguvu ya kijeshi kujaribu kuutanzua mgogoro unaoikabili, na kumtaka rais Bashar al-Assad kusimamisha mara moja vitendo vya ghasia. Tangazo hilo linaunga mkono umoja na mshikamano ndani ya Syria na kuheshimiwa kwa uhuru wa nchi hiyo.
Mvutano umekuwa ukiongezeka kwa miezi kadhaa baina ya Saudi Arabia ambayo wakazi wake wengi ni wa madhehebu ya Sunni, na Iran ambayo wengi ni washia, juu ya mzozo unaoendelea nchini Syria. Saudi Arabia inawaunga mkono waasi ambao wengi pia ni wasunni, dhidi ya serikali ya rais Bashar Assad yenye kudhibitiwa na waislamu wa kikundi cha Alawite, ambacho ni tawi la madhehebu ya washia. Iran imekuwa ikizishutumu Saudi Arabia, Qatar na Uturki kuwapatia silaha na fedha waasi.
Ishara njema ya maridhiano
Licha ya mivutano hiyo lakini, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad wameonekana kuweka kando tofauti zao katika mkutano huu, na mara kadhaa wamekuwa wakizungumza na kuangua kicheko. Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa Abdullah al-Shammari amesema hali hiyo inatuma ujumbe kwa watu wa nchi mbili kwamba licha ya tofauti zao, bado wote ni waislamu ambao wanaweza kufanya kazi pamoja.
Nchini Syria kwenyewe, mripuko mkubwa umetokea mjini Damascus karibu na hotel wanakokaa waangalizi wa Umoja wa Mataifa. Waasi wa Syria wamedai kuhusika na mripuko huo, na kusema kwamba walilenga mkutano wa kijeshi uliokuwa ukifanyika mahali hapo.
Shambulizi hilo limefanyika sehemu ambayo inazo hotel nyingi za kifahari, na pia kituo cha televisheni ya taifa na taasisi za usalama. Shambulio jingine la bomu lililofanywa mjini Damascus tarehe 18 mwezi Julai liliuwa maafisa wanne wa ngazi za juu za usalama, akiwemo waziri wa ulinzi. Televisheni ya taifa ya Syria imesema watu watatu wamejeruhiwa katika shambulio la leo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman