Tahadhari ya hali mbaya ya hewa yatolewa Ujerumani
13 Septemba 2024Inatarajiwa kuwa mvua yenye ukubwa wa hadi milimita 400 itanyesha katika milima ya mpakani kati ya Poland na Jamhuri ya Czech ndani ya muda wa saa 72, na itasababisha maafa katika miji na maeneo jirani.
Nchi zinazotarajiwa kuathiriwa katika siku zijazo ni pamoja na Poland, Ujerumani, Slovakia na Austria.
Soma pia:Mafuriko yasababisha uharibifu Ujerumani
Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Czech tangu Alhamisi, na inatarajiwa kuwa katika siku nne zijazo kiwango cha mvua katika maeneo yaliyoathiriwa kitakuwa zaidi ya theluthi moja ya kiwango cha mvua kinachorekodiwa mwaka mzima.
Poland imekuwa ikijenga vizuizi vya mafuriko katika kituo chake cha kihistoria mjini Prague baada ya idara ya utabiri wa hali ya anga ya Jamhuri ya Czech kutangaza mvua kubwa kunyesha hadi mji mkuu uliokumbwa na maafa mabaya, zaidi ya miaka 20 iliyopita.