1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban wateka mji mkuu wa pili wa jimbo Afghanistan

7 Agosti 2021

Kundi la Taliban limeteka ngome kuu ya mbabe wa kivita wa Afghanistan siku ya Jumamosi, wamesema maafisa, ukiwa mji mkuu wa pili wa jimbo kuangukia mikononi mwa waasi hao katika muda wa chini ya saa 24.

https://p.dw.com/p/3ygZ5
Afghanistan | Menschenmenge auf Fahrzeugen mit Taliban Flaggen in Chaman
Picha: Abdul Khaliq Achakzai/REUTERS

Mji wa Sheberghan ni nyumbani kwa mbabe wa kivita Abdul Rashid Dostum, ambaye amerejea  tu nchini Afghanistan wiki hii akitokea Uturuki alikokuwa anapatiwa matibabu.

Taliban wameyateka maeno makubwa ya vijijini nchini Afghanistan tangu kuanzisha mashambulizi mwezi Mei yaliokwenda sambamba na kuanza uondoaji wa mwisho wa vikosi majeshi ya kigeni.

Naibu gavana wa mji wa Sheberghan amesema wanajeshi wa serikali na maafisa walikimbilia kwenye uwanja wa ndege nje ya mji huo ulioko kaskazini mwa Afghanistan, ambako walikuwa wanajiandaa kujilinda.

Kwa bahati mbya mji umeangukia kikamilifu mikononi mwa Taliban," naibu gavana wa Jawzjan Qader Malia alisema.

Soma pia:Kundi la Taliban laudhibiti mji mkuu wa kwanza Afghanistan

Siku ya Ijumaa, mji wa Zaranj katika mkoa wa Nimroz uliangukia kwa Wataliban "bila mapigano" kwa mujibu wa naibu gavana, na kuwa mji mkuu wa kwanza wa jimbo kuchukuliwa na waasi hao.

Afghanistan | Konflikt mit Taliban
Moshi ukitanda katika mji mkuu wa jimbo la Jawzjan, kufuatia mapigano makali kati ya Taliban na vikosi vya serikali. Mji huo ulianguka siku ya Jumamosi.Picha: Mohammad Jan Aria/XinHua/dpa/picture alliance

Hakukuwa na upinzani Sheberghan, duru kadhaa zililiambia shirika la habari la AFP, lakini msaidizi mmoja wa Dostum alithibitisha kuwa mji huo umechukuliwa.

Dostum aliongoza mmoja ya kundi kubwa zaidi la wanamgambo kaskazini mwa Afghanistan, lililojipatia sifa ya kutisha katika mapambano yake dhidi ya Taliban katika miaka ya 1990 -- sambamba na shutuma kwamba vikosi vyake viliwachinja maelfu ya wafungwa wa kivita wa kundi hilo la waasi.

Soma pia: Taliban wanazidisha udhibiti kusini wa Afghanistan

Kushinda au kurudi nyuma kwa wapiganaji wake kutakuwa pigo kwa matumaini ya karibuni ya serikali mjini Kabul kwamba makundi ya wanamgambo yangesaidia kuimarisha jeshi la taifa lililozidiwa.

Mapokezi ya Taliban Nimroz

Roh Gul Khairazad, naibu gavana wa Nimroz, aliliambia shirika la habari la AFP Ijumaa kwamba Zaranj ilianguka "bila mapigano".

Picha na video kwenye mitandao ya kijamii zilionesha Wataliban walikaribishwa na baadhi ya wakaazi wa mji huo wa jangwani, ambao kwa muda mrefu umekuwa na sifa ya uhalifu.

Zilionesha magari ya kijeshi  na yale ya kifahari yaliokamatwa, yakiendeshwa kwa kasi mitaani, yakipeperusha bendera nyeupe za Taliban huku wenyeji -- wengi wao vijana na wanaume wenye umri mdogo -- wakiwashangilia.

Soma pia: Makomando wa Afghanistan wapambana na Taliban Herat

Moja ya mambo waasi hao walioyafanya baada ya kuingia Zaranj ilikuwa kufungua milango ya gereza la mji huo, wlaisema maafisa, na kuwaachia huru wafungwa wa Taliban pamoja na wahalifu wa kawaida.

Afghanistan Herat | Milizeinheiten nach kämpfen mit taliban
Wapiganaji binafsi wakitoa ulinzi baada ya vikosi vya usalma kukomboa baadhi ya maeneo ya mjkoa wa Herat kufuatia mapigano na Taliban, Agosti 6, 2021.Picha: Hamed Sarfarazi/AP/picture alliance

Vidio zilizowekwa kwenye mtandao wa Twitter zilionesha makundi yakifanya uporaji kwenye ofisi za serikali, wakiiba mabenchi, viti vya ofisini, makabati na televisheni. Uhalisia wa vidio hizo haukuweza kuthibitishwa mara moja.

"Vikosi vya usalama vya Afghanistan vilipoteza ari kutokana na propaganda kali kutoka kwa Taliban," alisema afisa mwandamizi kutoka mjini hapo, ambaye aliomba kutotajwa jina.

"Hata kabla ya mashambulizi ya Taliban.. sehemu kubwa ya wanajeshi waliweka chini silaha zao, wakavua sare zao, na kuacha vitengo vyao na kukimbia," alisema.

Soma pia: Mapambano ya kuwania mji wa Herat yaendelea Afghanistan

Serikali haijatoa tamko lolote rasmi bado kuhusu kuanguka kwa miji hiyo miwili. Kutekwa kwa Sheberghan kunakuja siku moja baada ya mkuu wa idara ya habari ya serikali kupigwa risasi na kuuawa mjini Kabul katika shambulizi ambalo Taliban walidai kuhusika nalo.

Baada ya jaribio lililoshindwa la mauaji dhidi ya waziri wa ulinzi wa nchi hiyo siku ya Jumanne, Taliabn walionya walikuwa sasa wanawalenga maafisa wandamizi wa utawala ili kulipiza kisasi kwa kuongezeka kwa mashambulizi ya angani dhidi yao.

Wataliban tayari wanadhibiti maeneo makubwa ya vijijini na sasa wanavikabili vikosi vya usalama katika miji mingine mikuu ya majimbo, ikiwemo Herat, karibu na mpaka wa magharibi na Iran, na Lashkar Gah na Kandahar kusini mwa nchi.

Kutokea Kunduz, mwanaharakarti Rasikh Maroof aliliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu Jumamosi, kwamba mapigano yalipamba moto usiku kwenye kingo za maeneo kadhaa ya mji, ambapo Wataliban walionekana kushindwa kupata mafanikio makubwa.

Washington | Präsident Ashraf Ghani
Rais wa Afghanistan Ashraf GhaniPicha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Vikosi vya serikali vilikuwa "vinalinda vikali," alisema, kwa kutumia mashambulizi ya angani dhidi ya maroketi ya Taliban na silaha nzito nzito.

White House yatetea uamuazi wa rais Biden

Licha ya hali inayozidi kudorora, msemaji wa ikulu ya Marekani White House jen Psaki, alisema Ijumaa kwamba rais Joe Biden alikuwa sahihi kuondoa vikosi vya Marekani baada ya vita vya miaka 20.

Marekani na Uingereza siku ya Jumamosi ziliwahimiza tena raia wake kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo.

Idadi ndogo ya wanajeshi wa Uingereza inatarajiwa kubakia Afghanistan kwa muda, lakini wanajeshi wengi zaidi wa tayari wameondoka.

Soma pia:UN: Wanawake na watoto waliuwawa zaidi Afghanistan

Wanajeshi wa mwisho wa mapambano wa Uingereza waliondoka Afghanistan Oktoba 2014. Na 750 tu ndiyo walibakia kama sehemu ya ujumbe wa NATO ili kutoa mafunzo wa vikosi vya serikali ya Afghanistan.

Kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni kunatazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa nane, kabla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani, ambayo yalisababisha uvamizi ulioliondoa madarakani kundi la Taliban.

Chanzo: Mashirika, DW