Tamasha kupinga wanazi lafanyika Ujerumani
4 Septemba 2018Bendi kadhaa maarufu nchini Ujerumani zilitumbuiza katika mji huo wa mashariki mwa Ujerumani kuwasilisha ujumbe kupinga vitendo vya kibaguzi kufuatia tukio la shambulizi la kisu dhidi ya mwanamme mmoja wa Ujerumani mnamo August 26. Wanaume wawili mmoja raia wa Iraq na mwingine wa Syria tayari wametiwa mbaroni wakihusishwa na tukio hilo.
Ni polisi 1,800 tu waliosambazwa katika mji wa Chemnitz hapo Jumamosi mnamo wakati jimbo la Saxony likishutumiwa kuruhusu polisi wachache katika maandamano Jumatatu.
Zaidi ya bendi tatu maarufu nchini Ujerumani ziliwatumbuiza waandamanaji hao wengi wao wakiwa ni vijana jana usiku wanaounga mkono uwepo wa wahamiaji nchini Ujerumani chini ya kauli mbiu isemeayo "SISI TUKO WENGI ZAIDI".
Maafisa wa mji wa Chemnitz walisema idadi ya watu waliohudhuria tamasha hilo jana usiku ni 65,000. Waandaaji wa tamasha hilo la jana walisema walitaka kuonesha kuwa hakuna nafasi katika mji wa Chemnitz kwa watu wenye mtizamo wa Kinazi.
Tamasha hilo liliungwa mkono na watu wengi
Hata hivyo tamasha hilo ilibidi lihamishiwe sehemu nyingine badala ya sehemu ya awali baada ya idadi ya watu wahudhuriaji kuongezeka.
Mmoja wa wanamuziki waliotumbuza kwenye tamasha hilo wa bendi ya Krraftklub alisikika akisema wao si watu wasiojitambua, huku akisisitiza kuwa wakati mwingine kuna haja ya kuonesha kuwa wahamiaji hawako peke yao.
Tamasha hilo lilianza kwa kukaa kimya kwa dakika moja kama ishara ya kumkumbuka mtu aliyeuawa katika shambulizi la kisu huku polisi wakisema hakukuwa na vurugu wakati wa saa za awali za tamasha hilo.
Maafisa wa mji wa Chemnitz waliwazuia wafuasi wa kundi la Pegida katika mji wa Chemnitz wasiandamane kupinga tamasha hilo.
Hayo yanajiri mnamo wakati watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa hadi sasa wakihusishwa na shambulizi la kisu wakihojiwa hapo jana ingawa msemaji wa upande wa mashitaka hakutoa maelezo zaidi.
Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinazodai kwamba mwanaume huyo aliyeuawa alikuwa akimlinda mwanamke mmoja wa Kijerumani dhidi ya washambuliaji ndizo zilizoibua ghadhabu katika baadhi ya vitongoji vya mji huo.
Mwandishi: Isaac Gamba/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef