TAMWA yazungumzia rushwa ya ngono kwa wanahabari wa kike
11 Septemba 2018TAMWA imesema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kituo cha sheria na haki za binadamu kutoa ripoti yake ya nusu mwaka inayoelezea hali ya haki za binandamu nchini Tanzania ambapo mbali na mambo mengine imeonesha kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono kwa waandishi habari wananawake.
Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waandishi wa habari wanawake Eda Sanga ameiambia DW kuwa, licha ya baadhi yao kukumbwa na kadhia hiyo ambayo inashusha utu wa mwanamke na kukiuka misingi ya binadamu, ukosefu wa sera ya usimamizi wa masuala ya ngono katika vyombo vya habari bado ni changamoto kubwa katika kukabiliana na tatizo hilo.
Hata hivyo tafiti mbalimbali za kidunia zinaonesha kuwa takriban asilimia arobaini na moja ya wanawake wanahababri na wasanii wanakumbana na visa vya kingono katika mazingira ya kazi, huku wananume ni asilimia ishirini na mbili, hii ikionyesha kuwa wanahabari wananwake wanaathirika zaidi kuliko wanaume.
Vichocheo vya rushwa ya ngono miongoni mwa wanahabari
Eda Sanga anaongeza kuwa kutokana na uzoefu wake katika tasnia ya habari, anasema kutokuwa na mapenzi ya dhati ya tasnia hiyo ni sehemu ya kichocheo cha kuongezeka kwa matukio ya rushwa ya ngono katika vyumba vya habari, ikiwemo na utendaji duni wa baadhi ya waathirika wa visa hivyo vya kingono.
Katika hili waandishi wa habari wanawake wanasema kuwa manyanyaso ya kingono katika vyumba vya habari bado yanashuhudiwa, hata baadhi hushushwa kiwango cha utendaji kazi wao kutokana na wao kukataa kutoa ngono, huku wengine wakidai kuwa wakati wa kuomba ajira hili linajitokeza zaidi.
Hili linatajwa kujitokeza katika vyombo vya habari mbalimbali ulimwenguni hata baadhi ya wanawake ambao wamekumbana na kadhia hiyo kuanzisha kampeni mbalimbali ambazo zinapinga vikali rushwa ya ngono na udhalilishaji wa kingono kwa waandishi wa habari wanawake katika vyombo vya habari, ikiwemo kampeni mashuhuri iliokwenda kwa jina la kimombo "me too” inayotajwa kuleta uthubutu wa kuzungumza kadhia za kingono kwa wanahabari wanawake kwa uwazi.
Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam
Mhariri:Josephat Charo