Tanzania: Magufuli akutana na viongozi wa upinzani
3 Machi 2020Viongozi wa vyama hivyo vya upinzani wamekaribishwa ikulu kwa nyakati tofauti na picha za vidio zilizotolewa na Ikulu zinamwononesha mwanasiasa wa siku nyingi na mshauri mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif akifurahia jambo na Rais Magufuli na wawili hao wakionekana kuwa katika hali ya bashasha kubwa.
Maalim Seif aliyewania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF zaidi ya mara tatu, akilalamika kupokwa ushindi wake ameutaja mkutano wake wa Jumanne na Rais Magufuli kuwa ni wa mafanikio makubwa.
"Namshukuru rais kwamba kakubali tukutane tuzungumze mambo ya maslahi ya nchi yetu. Namshukuru sana,"amesema Sharif.
Mbali na Maalim Seif, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa wengine. Na kulingana na picha zilizotolewa na Ikulu, amekutana na Mwenyekiti wa chama cha wananchi Cuf, Profesa Ibarahim Lipumba na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia.
Hakuna picha yoyote ya vidio iliyotolewa kuwaonyesha wanasiasa hao wawili wakizungumzia mkutano wao na Rais Magufuli, lakini alipokutana baadaye na waandishi wa habari katika ofisi za chama chake, mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi Mbatia alidokeza baadhi ya mambo aliyojajadili wakati akiwa Ikulu. Amesema suala kuhusu uchaguzi mkuu ujao ni miongoni mwa mambo ambayo yalijadiliwa kwenye mkutano huo.
"Leo nimeitwa na mheshimiwa rais nimemuuliza nchi hii tunaipeleka wapi? Akaniambia kama nilivyowaambia mabalozi, ninaendelea kusisitiza uchaguzi wa mara hii utakuwa ni wa huru na wa haki, " ameeleza Mbatia.
Hadi sasa bado haijafahamika kama viongozi wa vyama vingine vya siasa wameitwa Ikulu ikiwamo chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho mara zote kimekuwa kikiimba wimbo wa kutaka tume huru kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Mikutano hiyo ya Rais Magufuli huenda ikawa hatua muhimu ya kukaribisha maridhiano ya wanasiasa hasa wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu.
Suala la kutaka maridhiano ya kitaifa limewahi kuibuliwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati chama chake kilipohudhuria na kushiriki kwa mara ya kwanza kilele cha sherehe za uhuru wa Tanganyika zilizofanyika Disemba 9 jijini Mwanza.