1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Tanzania kujadili ripoti ya CAG Novemba

George Njogopa14 Aprili 2023

Hatua ya Bunge la Tanzania kuamua kwamba mjadala jumla wa bunge kuhusu yale yaliyoanikwa katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) utafanyika mwezi Novemba, yazusha hasira

https://p.dw.com/p/4Q58A
Spika wa Bunge la Tanzania Dr. Tulia Ackson
Spika Ackson amesema kamati za bunge ziwasilishe kwanza ripoti zaoPicha: Ericky Boniphace

Hatua ya  Bunge la Tanzania kuamua kwamba mjadala jumla wa bunge hilo kuhusu yale yaliyoanikwa katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) utafanyika mwezi Novemba, inaonekana kuwakasirisha wengi huku baadhi ya wakosoaji wa mambo wakitaja mapungufu ya sheria yanayotoa mwanya wa ripoti hiyo kutojadiliwa kwa wakati baada ya kutolewa kwa umma.

Soma pia: Tanzania: Ripoti ya CAG yazusha joto bungeni

Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Wabunge wataijadili kwa kina ripoti ya CAG NovembaPicha: DW/S. Khamis

Spika wa Bunge, Akson Tulia ametangaza kwamba mjadala wa ripoti hiyo utafanyika mwezi Novemba baada ya kamati za bunge kuwasilisha ripoti zao, lakini hatua hiyo imeamsha hasira na kuwakera wengi wanaona kwamba inatoa mwanya kwa wale waliotaja ndani ya ripoti hiyo kuwa katika mazingira mazuri ya kujipanga.

Huku wengine wakitoa mapendekezo ya kurekenbisha kasoro hiyo, lakini idadi kubwa wanaonekana kuvunjika moyo hasa kwa kuzingatia ubadhilifu mkubwa uliofichuliwa ndani ya ripoti hiyo ambayo wahusika wake wakumbwa ni watendaji wa serikali.

Akilizatama suala hilo, mchambuzi wa masuala jumla, Gwantumi Mwakatobe anaona kwamba kutua muda zaidi kwa ripoti hiyo kujadili na bunge ni sawa na kumsogezea sahani ya mlo mtu ambaye tayari alishaketi mezani na kumaliza chakula chote.

Maoni ya Watanzania kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG

Miito ya kutaka wale wote waliotajwa kwenye ripoti ya CAG kuwajibishwa haraka iwezekanavyo inaendelea kusikika katika mijadala mbalimbali kuanzia ile inayohusisha vyama vya kisiasa, makundi ya kijamii pamoja na makundi ya wasomi.

Mtaalamu wa masuala ya sheria, wakili wa siku nyingi, Dr Rugemeleza Nshala akichambua kwa nini wale wanaochelewa kuwajibishwa licha ya kutuhumiwa na ripoti hiyo, amewarai wananchi kuanza kupasa suati akisema ndiyo wahusika wa rasimali za taifa.

Wakati akieleza sababu za ripoti hiyo kujadiliwa na bunge katika kipindi cha mwezi Novemba, spika wa Bunge hilo, Tulia alisema hatua hiyo imelenga kutoa muda kwa kamati mahsuisi za bunge hilo kuipitia na kisha kuwasilisha mapendekezo yake bungeni.

Wakati vuguvugu kuhusu mjadala wa ripoti ya CAG ukiwa bado umeshika kasi, Rais Samia Suluhu Hassan na makamu wake wameahidi kuwawajibisha wale wote waliohusika katika ubadhilifu wa mali ya umma.