Tanzania: Ukeketaji sasa unafanywa kwa vichanga
6 Februari 2024Katika taarifa iliyotolewa na Mtandao wa asasi 12 za kupinga ukeketaji nchini humo, wadau hao wamesema, licha ya jitihada zinazofanywa na serikali, mashirika na taasisi, bado mila hiyo kandamizi ya ukeketaji inaendelea.
Takwimu za Demografia ya Afya za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa, asilimia 10 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wamekeketwa Tanzania wakati takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha idadi hiyo imepungua kwa asilimia 2 tu ambapo kwa sasa ni asilimia 8 ya wanawake wa umri huo wamekeketwa.
Mtandao huo umesema, wakeketaji wanabuni mbinu mpya na sasa wanawakeketa watoto wachanga.
Ukeketaji waripotiwa kwenye mikoa ambayo kabla haukuwepo
Kwa mujibu wa wanamtandao huo, ukeketaji wa watoto wachanga, ni ukatili mbaya unaoanza kupoteza haki za watoto wa kike wakiwa na umri mdogo zaidi.
Takwimu za demografia ya afya za mwaka 2022 zimeonyesha kuwa mikoa inayoongoza kwa ukeketaji Tanzania ni Arusha,asilimia 43, Manyara (43), Mara asilimia 28 na Singida 20.
Hata hivyo wadau hao wamesema, kuna mikoa ambayo awali haikuwa na ukeketaji lakini takwimu mpya zinaonyesha kuanzia mwaka 2022 wameanza kufanya ukeketaji.
Siku ya Kupinga ukeketaji hufanyika Februari 6 kila mwaka, ambapo Umoja wa Mataifa, uliitambua rasmi siku hii baada ya kuona athari za ukeketaji kwa watoto wake. Kauli mbiu kwa mwaka ni "Sauti yake Hatima yake; Wekeza kwa manusura kutokomeza Ukeketaji”