1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Wabunge wa EALA wachaguliwa

Deo Kaji Makomba
22 Septemba 2022

Nchini Tanzania uchaguzi wa wabunge wa bunge la Afrika mashariki watakaoiwakilisha nchi hiyo katika bunge hilo umekamilika kwa wabunge tisa kuchaguliwa

https://p.dw.com/p/4HDRR
 East African Community Headquarters in Arusha, Tanzania
Bunge la Afrika Mashariki lipo ArushaPicha: Veronica Natalis/DW

Uchaguzi huo umeendeshwa kwa utaratibu wa makundi ambapo wagombea katika nafasi hizo za uwakilishi katika bunge la Afrika Mashariki  waligawanywa katika makundi  A, B na C , wakiwa ni kutoka CCM, vyama vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni na wawakilishi kutoka Zanzibar.

Mara baada ya kukamilika zoezi la kupiga na kuhesabu kura Spika wa bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, akatangaza matokeo ya uchaguzi huo wa wabunge watakaoiwakalisha Tanzania katika bunge la Afrika Mashariki,mjini Arusha.

Tansania Dr. Tulia Ackson
Spika wa Bunge la Tanzania Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Awali wagombea katika nafasi hizo za uwakilishi kwenye bunge la Afrika Mashariki walijinadi kwa kutumia lugha ya kiingereza kama ilivyo ada kwa wagombea wa nafasi hizo huku maswali pia kwa lugha ya kiingereza yakiulizwa na wabunge, akiwemo mbunge wa Geita vijijini Joseph Kasheku Msukuma.

Hata hivyo kitendo cha wagombea wa nafasi za uwakilishi katika bunge la Afrika Mashariki kujinadi kwa  lugha ya kiingereza limezua mjadala mkubwa nchini Tanzania na katika mitandao ya kijamii huku wachangiaji katika mitandao wakiwa na maoni haya.

Suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Tanzania, limekuwa likihimizwa kutumika ili kuendelea kuitangaza lugha hiyo kitaifa na kimataifa lakini bado baadhi ya sekta nchini humu zimekuwa zikitumia lugha ya kingereza kama lugha ya mawasiliano.

Deo Kaji Makomba/DW Dodoma