Tanzania yakosolewa kwa kutotoa taarifa za corona
13 Mei 2020Mara ya mwisho Tanzania kutoa taarifa ya watu waliokumbwa na maambukizi hayo ilikuwa na Aprili 29 na hadi leo inapofika Mei 13, hakuna taarifa zozote zilizotolewa na serikali kuhusu watu waliofikwa na mkasa huo.
Hadi sasa ni vigumu kubashiri idadi jumla ya watu waliokumbwa na maambukizi hayo wala idadi ya watu waliopoteza maisha, ingawa shughuli za kijamii na zile za kiuchumi zimekuwa zikiendelea kama kawaida, ukiachilia mbali kufungwa kwa shule, vyuo na shughuli za michezo.
Makundi ya wanasiasa pamoja na wachambuzi wa mambo wamekuwa wakitupa lawama kwa mamlaka za kiutendaji wakisema inachukua mwendo wa kinyonga kutoa taarifa kamili kuhusiana na mwenendo jumla wa maambukizi ya virusi hivyo, na wamekuwa wakikosoa kuhusu mipaka yake kuendelea kuwa wazi.
Karibu mataifa yote jirani na Tanzania yamekuwa yakiongeza udhibiti katika mipaka yake na katika siku za karibuni mataifa hayo yameonyesha kuchukua hatua kubwa zaidi kwa kuwabana raia wa Tanzania wanaotaka kuingia nchini humo hasa madereza wa magari makubwa wanaozuiliwa ama kuamuliwa kufanyiwa vipimo vya lazima.
Kumekuwa na madai kuwa huenda Tanzania imetengwa na nchi washirika katika ukanda wa Sadc na Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na namna mataifa hayo yanavyochukua maamuzi yanayofanana katika kushughulikia kadhia ya janga hilo.
Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Prof Palamagamba Kabudi akisema tuhuma kuwa nchi hiyo imelegalega ama kujitenga katika mapambano dhidi ya corona siyo ya kweli.
Kabudi amesema badala yake, Tanzania ikiwa kama kiongozi wa SADC imetoa uongozi madhubuti katika kukabiliana na janga hilo kwenye ukanda huo. Naye waziri wa afya, Ummy Mwalimu amekuwa akipuzilia mbali taarifa zinazosema Tanzania inaficha taarifa za ukweli kuhusu maambukizi ya janga hilo.
Amenukuliwa akisema kwa sasa kunafanyika hatua kadha wa kadha za kuboresha maabara ya taifa na baada ya hapo taarifa zitaendelea kutolewa.
Hivi karibuni Waziri huyo aliwasimamisha kazi maofisa wa maabara ya taifa na kuunda timu ya wataalamu kuchunguza utendaji wa maabara hiyo baada ya Rais John Magufuli kutilia shaka uwezo wa mitambo inayotumika kupima virusi hivyo vya corona.
Katika hatua nyingine ya kukabiliana na athari ya janga hilo, Benki Kuu ya Tanzania imetoa maelekezo kwa mabenki na makampuni ya simu juu ya namna ya kutoa unafuu wa masuala ya kifedha kwa wateja wao.
Benki Kuu imeyaagiza mabenki yote nchini kufanya mjadala na wateja wao juu ya urejeshwaji wa mikopo na kutafuta namna nafuu ya urejeshaji wa mikopo hiyo.
George Njogopa.