Tanzania yalegeza masharti ya COVID-19
17 Machi 2022Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa kuanzia leo inalegeza rasmi masharti kwa wageni wanaotaka kuingia nchini humo ambao watakuwa tayari wametimiza masharti ya COVID-19.
Kwa maana hiyo msafiri yeyote aliyechanja dhidi ya virusi vya corona anaondolewa masharti ya kuonyesha cheti cha vipimo kuthibitisha kutokuwa na corona.
Awali taifa hilo la Afrika Mashariki liliweka masharti likiwataka wasafiri wote wanaoingia nchini humo kuonyesha vyeti vikithibitisha wamechanjwa na hawana maambukizi ya COVID-19.
Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amewaagiza maafisa wa afya pamoja na watendaji wengine wa serikali kuhakikisha agizo hilo la ulegezaji masharti linatekelezwa na kuondoa bugudha yoyote katika maeneo ya mipakani.
Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema licha ya chanjo kuendelea kuwa ni jambo la hiari, amewahimiza wananchi kutambua umuhimu wake.