Tanzania yatuhumiwa kuzuia huduma za jamii Ngorongoro
19 Aprili 2022Kwanza zilianza tetesi za kuwepo kwa mipango ya kuwakatisha tamaa wakazi wa hifadhi ya taifa ya Ngorongoro kwa kuwanyima huduma muhimu za kijamii lakini baada ya tetesi, ilisambaa barua kutoka Tawala za mikoa na serikali za Mitaa, (TAMISEMI) iliyoelekezwa kwa walimu wa shule za sekondari wilayani humo ikiwataka wakuu wa shule hizo kurudisha fedha za UVIKO 19 kiasi cha Sh 19.6 bilioni zilizopangwa kutumika kukarabati shule na badala yake wazielekeze katika akaunti ya benki ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.Tanzania yafafanua kuhusu sakata la Ngorongoro
Hatua hizo zimetafsiriwa kama mbinu za kuwaondosha wakazi hao katika eneo hilo. Mwenyekiti wa Wazee wa Kimila wilaya ya Ngorongoro, tarafa ya Ngorongoro, maarufu kama Laigwanak, Metui Ole Shaudo amesema kuwa "kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa shule, vituo vya afya na shule ya sekondari vimesimama".
Awali, Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kinachoendelea wilayani humo ni uvunjifu wa haki za binadamu na ni doa linalokwenda kumchafua Rais Samia Suluhu Hasan.
Ole Ngurumwa amesema ni vyema kama wananchi wakashirikishwa ili haki zao zizingatiwe na uhifadhi uendelee na akaongeza zaidi kuwa, ni bora iwepo mikakati kutafuta suluhu na wananchi badala ya kuamua kuzuia huduma za kijamii kuwa fimbo ya kuwaondoa wakazi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala alipoombwa na idhaa hii kuzungumzia tuhuma hizo hakupenda kuzigusia, badala yake alitaka atafutwe baadaye kwa sababu wakati huo alikuwa vijijini akikagua miradi ya maendeleo.
Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 na serikali ya kikoloni baada ya watu wa kabila la Maasai kuhamishwa kutoka hifadhi ya Serengeti. Hata hivyo, baada ya Ngorongoro kuwa hifadhi mseto ya wanyama na binadamu kwa muda mrefu, kumekuwapo na mipango ya kuwahamisha tena wakazi hao.