1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Teknolojia mpya na uwakilishi wa Afrika kwenye CeBIT 2005

Richard Madete15 Machi 2005

Maonyesho ya wiki moja ya kompyuta na njia za mawasiliano ya kisasa CEBIT, ambayo huyavutia makampuni na wageni wengi kutoka nchi za nje, yanaendelea mjini Hannover. Kama kawaida, bara la Afrika nalo huwakilishwa kwenye maonyesho haya kwa makampuni mbalimbali, kwa mfano mara hii kuna wawakilishi kutoka Afrika-Kusini, Kenya na Misri.

https://p.dw.com/p/CHhE
CeBIT 2005 - Simu ya mkononi inatumiwa kama kioo pia
CeBIT 2005 - Simu ya mkononi inatumiwa kama kioo piaPicha: AP

Maonyesho ya kompyuta na njia za mawasiliano ya kisasa ni uwanja wa makampuni kutoka duniani kote kuonyesha bidhaa wanazotengeneza na zile wanazotarajia kutengeneza hapo baadaye.

Mwelekeo wa muda mrefu wa vifaa vya mawasialiano kuzidi kuwa kitu kimoja, kuongeza ufanisi na hapohapo kuwa vidogo zaidi, umeendelezwa hata kwenye maonyesho ya mwaka huu.

Mkurugenzi wa shirika linaloandaa maonyesho haya, Ernst Raue, amenukuliwa akisema, vifaa vya kompyuta zinazidi kuuunganishwa na vifaa vya mawasiliano pamoja na vifaa vya burudani.

Na ndiyo maana, kwa kutumia teknolojia mpya ya UMTS, simu ya mkononi hivi sasa inaweza kutumiwa kwa mambo mengi; kama chombo cha mawasiliano, kompyuta na hapohapo kama chombo cha burudani, kusikiliza muziki, kupiga picha au hata kuangalia video.

Simu za mkononi kwa mfano simu moja ya SONY-ERICSSON iliyoletwa hapa kwenye maonyesho ya CEBIT, inaweza kutumiwa kwa mambo yote hayo pamoja na kufanya mazungumzo kwa njia ya video. Na inaweza kuwasiliana na kompyuta na vifaa vingine kwa kutumia teknolojia mpya ya Bluetooth.

Zaidi ya maonyesho ya CEBIT kutumiwa kama uwanja wa kuonyesha teknolojia za siku za usoni, makampuni mengi huja kwenye maonyesho haya ili kuonyesha bidhaa za kufanyia kazi za kawaida katika ofisi na kwa watu binafsi.
Zaidi ya makampuni 6 ya kutengeneza vifaa mbalimbali vya simu kutoka Misri yamewakilishwa hapa. Pia zaidi ya makampuni 10 kutoka Afrika-Kusini yamefika kwenye maonyesho ya mwaka huu.

Kwa mfano kampuni la Afrika-Kusini liitwalo FUNDAMO limekuja kutafuta soko la programu zake za kufanyia malipo kwa njia ya simu za mkononi. Kama yanavyofanya makampuni mengi kutoka nchi zinazoendelea, makampuni yote kutoka Afrika-kusini, yanatumia banda moja ili kupunguza gharama.

Nilimhoji kiongozi wa msafara huu kutoka Afrika Kusini bwana Vusi Mweli kuhusu mpango huu akasema, serikali inalipa gharama zote kwa lengo la kuyasaidia makampuni ya uwezo wa kati, kupata masoko katika nchi za viwanda. Wamekuwa wanafanya hivi kwa mafanikio makubwa tangu miaka minne hivi iliyopita.

Kenya inaandaa mkutano na maonyesho ya kimataifa ya Kompyuta, ICTE – AFRICA, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Mei mwaka huu. Mkutano huu unahusu pia maandalizi ya Afrika kwenye mkutano wa kimataifa wa kompyuta na njia za mawasiliano. Wahusika wametumia maonyesho ya CEBIT kutangaza na kutafuta makampuni ya nchi za viwanda kwenda kushiriki kwenye mkutano na maonyesho hayo ya aina yake barani Afrika.

Kwa upande wa teknolojia mpya za kompyuta, makampuni mbalimbali mwaka huu yamekuja kuonyesha teknolojia za kupunguza kelele kwenye kompuyta, hadi kufikia kipimo cha Decibles 40. Kompyuta zisizo na kelele – no noise computer - zinazopozwa kwa maji kama magari badala ya feni ni mojawapo ya teknolojia za kompyuta iliyotia fora mwaka huu.

Kampuni la Ujerumani ALPHACOOL GmbH linaonyesha kompyuta inayotumia teknolojia iliyofanyiwa utafiti kwenye maabara zao na kwenye chuo kikuu cha Bayreuth. Kampuni hili linatengeneza vifaa vya kupozea processor na graphic card kwenye kompyuta za kawaida ili kupunguza kelele. ALPHACOOL imejipatia tuzo nyingi kwa tekonojia na vifaa vyake vinavyouzwa katika nchi 27 duniani.