Akili Mnemba kusaidia kuhifadhi nyaraka za enzi ya ukoloni
13 Agosti 2024Yeyote anayelenga kufanya utafiti wa kina katika kumbukumbu za Ujerumani za kabla ya Vita vya Pili vya Dunia, anahitaji kuwa na ujuzi na kuwa na uwezo wa kusoma aina fulani za mwandiko ambazo kwa sasa zimetoweka kabisa katika matumizi ya kila siku katika lugha ya Kijerumani.Bunge la Ulaya laidhinisha sheria za kusimamia teknolojia ya AI
Kuna "Kurrent", aina fulani ya uandishi iliyotumiwa hapo awali pamoja na aina tofauti tofauti, haswa "Sütterlin" iliyotumiwa kwa muda mfupi. Aina hii ya uandishi ilianzishwa mwaka 1911 na kufundishwa katika shule za Ujerumani kuanzia mwaka 1915 hadi 1941, hadi ilipopigwa marufuku na watawala wa Kinazi. Baadaye, watoto katika shule hizo walijifunza mwandiko unaoshabihiana na maandishi ya Kiingereza.
Soma: Kampuni ya Woermann ilivyousafirisha ukoloni wa Ujerumani
Ingawa wazungumzaji wa Kijerumani ambao waliwahi kutumia aina ya maandishi ya Sütterlin waliendelea kuitumia vyema hadi katika kipindi cha baada ya vita vya Pili vya Dunia, Wajerumani wengi hawawezi kusoma nyaraka zilizoandikwa na babu na bibi zao. Lakini sasa, programu ya akili mnemba (AI) inaweza kuwasaidia kwa hilo.
Zana mpya imetengenezwa na Hifadhi ya Kumbukumbu ya Shirikisho la Ujerumani (Bundesarchiv) ili kusaidia kufafanua aina tofauti za maandishi zinazoweza kupatikana katika hati za enzi ya ukoloni.
Hata hivyo nyaraka nyingi muhimu bado zinahitaji kufanyiwa kazi
Hati za enzi ya ukoloni zilikuwa muhimu mno kwa mradi kama huo, kwa kuwa Hifadhi ya Kumbukumbu ya Shirikisho la Ujerumani inamiliki mkusanyiko wa nyaraka zipatazo 10,000 kutoka kwenye Ofisi ya Ukoloni ya Reich, ambayo ndiyo iliyokuwa na mamlaka kuu ya kusimamia sera ya ukoloni ya Dola ya Ujerumani.
Msemaji wa Hifadhi ya kumbukumbu, Elmar Kramer, ameiambia DW kuwa walichaguwa nyaraka hizo za enzi ya ukoloni kwa sababu sehemu kubwa iliandikwa kwa mkono.
Soma: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"
Lakini meneja wa mradi huo Inger Banse amesema mkusanyiko huo ulichaguliwa kuwa kwenye mpango wa majaribio kwa sababu nyaraka zote kutoka Ofisi ya Ukoloni ya Reich tayari zimehifadhiwa kidijitali na hazina vizuizi vyovyote kwa watumiaji.
Muhimu zaidi, kama anavyoelezea Banse ni kukubaliana na historia ya enzi za ukoloni kwa kuwa jamii nzima inatilia maanani suala hilo, na hivyo wanaweza kutoa mchango mzuri kutokana na mkusanyiko wa nyaraka hizo.
Kamishna wa Utamaduni na Vyombo vya Habari wa Ujerumani Claudia Roth, wakati akipongeza mradi huo wa Hifadhi ya Shirikisho wa kutumia teknolojia maalum ya akili mnemba (AI) amesema kwa muda mrefu sana, uhalifu wa Ujerumani wakati wa enzi ya ukoloni ulikuwa umefichwa katika tamaduni za ukumbusho, lakini teknolojia hii itaimarisha ujuzi kuhusu matukio hayo mabaya katika historia ya Ujerumani, na kwamba kufanya hivyo, ni kutoa mchango muhimu katika kukubaliana na yaliyotokea.
Mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20
Ukoloni wa Dola ya Ujerumani ulianza mwishoni mwa karne ya 19 na ulilenga zaidi kumiliki maeneo na kuanzisha makoloni barani Afrika, katika maeneo ya Bahari ya Kusini pamoja na China.
Utawala wa kikoloni wa Ujerumani ulidumu kwa miaka 30 tu, kuanzia mwaka 1884 hadi mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Duni, lakini muda mfupi tu baada ya kuanzishwa kwake, ulikuwa ni utawala wa Kikoloni ulioshikilia nafasi ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya ule wa Uingereza na Ufaransa. Na utawala wa kikoloni wa Ujerumani ulikuwa wa kikatili mno.Wataalam TZ walalamikia kukosekana sera ya Akili Mnemba
Jambo la kuchukiza zaidi ni kwamba Ujerumani ilitenda mauaji ya kimbari ya jamii za Herero na Nama, yanayojulikana kama mauaji ya halaiki ya kwanza ya karne ya 20. Yalifanyika kuanzia mwaka 1904 hadi 1908, baada ya jamii hizo kuanzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kijerumani. Ni mwaka 2021 tu ndipo Ujerumani ilikubali rasmi kuwa ilifanya mauaji ya kimbari wakati wa ukoloni wake katika eneo ambalo kwa sasa ni taifa la Namibia.