1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliokufa kwa tetemeko la Morocco, yafikia 2,122

11 Septemba 2023

Timu za waokozi kutoka mataifa ya Uhispania, Uingereza na Qatar zimeanza kazi ya kuisadia Morocco katika maeneo ambayo yamethiriwa na tetemeko la ardhi katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika

https://p.dw.com/p/4WBqW
Marokko nach dem schwerem Erdbeben
Picha: Khalifa bin Hamad Al Thani/AFP

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Morocco, MAP, Uingereza imepeleka waokozi 60 pamoja na vifaa vya kutafuta miili ya watu, wakiwemo mbwa wanne ambao watashiriki operesheni ya uokozi inayoongozwa na Wamoroko wenyewe. Taarifa hiyo amenukuliwa Balozi wa Uingereza nchini humo, Simon Martin ambayo ameiandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulifahamika kwama Twitter.

Awali Jumapili, ilionesha kupata ahadi hiyo ya msaada iliyotolewa na taifa hilo, Uingereza sambamba na Uhispania, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE. Mataifa hayo yalipendekeza kuunda kundi la utafiti na uokozi. Baadae serikali ya mjini Rabat ilisema itaweza kupokea ahadi ya usaidizi ambayo imetolewa na watu wengine.

Hali ya dharura katika kukabiliana na athari

Mustapha Baitas, ambae ni msemaji wa serikali ya Morocco alisema "Mheshimiwa Mfalme ataongoza kikao cha kamati ya wizara inayohusika na kuandaa mpango wa dharura wa kutoa msaada na kujenga upya nyumba zilizoharibiwa katika maeneo yaliyoathirika haraka iwezekanavyo."

Marokko | Erdbeben in Marokko
Waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Morocco.Picha: FADEL SENNA/AFP

Mapema Asubuhi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna amesema Morocco ina uhuru wa kuchagua kama inataka msaada wa Ufaransa katika kushughulikia janga hilo la tetemeko la ardhi, ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa takribani kipindi cha miongo sita. Amesema taifa lake lipo tayari kutimiza pale litakapoombwa.

Serikali za Paris na Rabat zimekuwa katika uhusiano mbaya katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na suala la Sahara Magharibi, ambapo Morocco inaitaka Ufaransa ilitambue eneo hilo kuwa ni sehemu yake. Pamoja na hayo Ufaransa imeahidi kutoa Euro milioni 5 kwa asasi za kiraia zinazohudumu Morocco.

Idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka zaidi

Zaidi ya watu elfu mbili wamekufa kufuatia tetemeko hilo la Ijumaa lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter, ambalo limeyaathiri maeneo mengi ya Morocco. Tetemeko hilo limesababisha kuporomoka kwa miamba, kuzuia barabara, hali iliyosababisha ugumu kwa shughuli za timu za uokozi kuyafikia maeneo ya milimani ambayo yameathirika kwa kiwango kikubwa.

Waokoaji wamekuwa na changamoto ya kufika katika maeneo ya watu walionusurika kwa wakati, katika kazi yao hiyo inayokabiliwa na changamoto kubwa. Kwa mujibu wa wanaoshuhudia hali ilivyo sasa nchini humo, hadi jana Jumapili, baada ya maeneo yaliyoathiriwa yameonekana kutengwa kutokana na kufunikwa na maporomoko ya ardhi.

Soma zaidi:Zaidi ya watu 1,000 wamefariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi nchini Morocco

Na baadhi ya watu walionusurika wanasema harufu ya miili ya watu waliopoteza maisha imeanza kusikika kutoka chini ya vifusi.

Vyanzo: RTR