Kisa hiki cha tetemeko la ardhi huenda pia kikagubika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei na ambao tayari unaonekana kuwa mgumu kabisa katika kipindi cha miongo miwili ya utawala wake.
Siku moja baada ya tetemeko hilo lililosababisha maafa makubwa nchini Uturuki, wanasiasa wa upinzani na baadhi ya wakazi katika maeneo yaliyoathirika zaidi walilalamika kwamba mamlaka zilikuwa zinajikongoja ama zilikuwa hazijiwezi kabisa kukabiliana na janga hilo kubwa kabisa.
Soma Zaidi: Erdogan akiri changamoto kwenye shughuli za uokozi
Na fikra yoyote inayoashiria serikali kushindwa kushughulikia majanga kikamilifu ama kushindwa kuzingatia miongozo ya ujenzi mpya kwenye maeneo yaliyoathirika na tetemeko, inaweza kumuathiri pakubwa Erdogan katika uchaguzi huo.
Lakini wachambuzi wanasema rais huyo, mwenye uzoefu mkubwa wa kufanya kampeni na ambaye tangu alipoingia madarakani mwaka 2003 serikali yake imeweza kukabiliana na matetemeko, mioto ya mwituni na majanga mengine ya asili anaweza kwa mara nyingine kuwashawsihi wapiga kura kumuunga mkono katikatika ya janga hili la sasa na hivyo kujiimarisha zaidi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi huo.
Alipozungumza masaa kadhaa baada ya tetemeko hilo la Jumatatu ambalo ni baya zaidi kuipiga Uturuki katika kipindi cha miaka 80, Erdogan alisema maelfu ya wafanyakazi wa uokozi tayari walikuwa wamekwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na kuwahakikishia watu ya kwamba hakuna kitakachozuia juhudi za uokozi, japo majira ya sasa ni baridi kali.
Mshauri mmoja wa shirika linalojihusisha na ushauri la Eurasia Group consultancy amesema Erdogan amefanikiwa kulishughulikia kwa usawa na kwa haraka janga hilo. Na ni hakika linamuweka mahali pazuri kulekea uchaguzi huo wa Mei 14, lakini iwapo tu serikali yake itaendeleza kasi hiyo.
'KIWINGU CHEUSI'
Ujenzi mpya unatarajiwa kugharimu mabilioni ya dola, hali inayoweza kuongeza hali ngumu kwenye uchumi ambao tayari umezorota, wakati kukishuhudiwa mfumuko wa bei uliofikia asilimia 58 na athari za tetemeko katika eneo linalokaliwa na wakazi milioni 13 pia zinatarajiwa kudidimiza hata zaidi ukuaji wa uchumi, hii ikiwa ni kulingana na wataalamu wa uchumi.
Atilla Yesilda, mtaalamu wa uchumi na siasa katika taasisi ya Global Source Partners anayelifananisha janga hilo na ndege mweusi anasema ni wazi kwamba litakuwa na athari kubwa mno na kuongeza kuwa hata hadhani kama uchaguzi utafanyika kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi.
Wapinzani wa kisiasa wa Erdogan bado hawajaanza kuzitumia athari za janga hilo kujiimarisha kisiasa. Bado wanavuta subira katika kipindi hiki ambacho bado wengi wamekwama chini ya vifusi na idadi ya vifo ikizidi kuongezeka. Muungano wa upinzani unaokutanisha vyama sita wenyewe uliitolea tu mwito serikali kushughulikia janga hilo bila ubaguzi na hasa kwenye maeneo yanayokaliwa na watu wa jamii ya Kikurdi na wakimbizi wa Syria.
Lakini wakati vyama hivyo vikitoa mwito huo, katibu mkuu wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha IYI, Ugur Poyraz alinukuliwa akisema alitembelea baadhi ya maeneo yaliyaothiriwa zaidi na hadi siku ya Jumanne asubuhi hakukuwa hata na dalili ya kupelekewa wafanyakazi wa uokozi.
Hasnain Malik, mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa utafiti wa uwekezaji na takwimu wa Tellimer ulioko Dubai anasema namna serikali inavyoshughulikia janga hili ndivyo itakavyojifungulia milango ya kura kutoka kwa matabaka ya watu wa kipato cha kati kwenye maeneo yaliyoathirika, ingawa haitakuwa rahisi kwa wapiga kura wenye misimamo ama wafuasi kindakindaki waliopo ama kwenye maeneo hayo yaliyoathirika ama yaliyo salama.