Shughuli za uokozi zaendelea usiku kucha Uturuki na Syria
8 Februari 2023Wafanyakazi wa vitengo vya dharura wa Uturuki na Syria wanaungwa mkono na wengine kutoka duniani kote, huku msaada wa kimataifa ukiendelea kuwasili. Maafisa wanasema idadi ya waliouawa na tetemeko la Jumatatu imefika watu 7,926 katika nchi hizo mbili.
Soma zaidi: Erdogan atangaza hali ya dharura katika maeneo ya tetemeko
Makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay alisema jana Jumanne kwamba watu 5,894 wameuawa na 34,810 wamejeruhiwa nchini Uturuki, wakati shughuli za utafutaji zikiendelea takribani saa 48 tangu tetemeko la kwanza kutokea.
Nchini Syria, shirika la habari la serikali SANA liliripoti kuwa watu 812 wameuawa na 1,449 kujeruhiwa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali. Shirika la White Helmet linaloratibu juhudi za uokoaji katika eneo linaloshikiliwa na waasi limesema watu 1,220 waliuawa na 2,600 kujeruhiwa.
Jumuiya ya kimataifa yajitolea kusaidia
Timu za waokoaji kutoka Korea Kusini, Marekani, Bosnia-Herzegovina, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu -hizo zikiwa baadhi tu ya nchi zilizotuma msaada - zimejiunga na oparesheni za kuwatafuta watu chini ya kifusi, huku matumaini ya kuwapata walio bado hai yakiendelea kufifia.
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani, USAID, limesema vikundi viwili vya wataalamu wake wa uokoaji zimewasili Uturuki mapema Jumatano.
Soma zaidi: Nchi duniani kote zinahamasisha misaada ya haraka kwa ajili ya Syria na Uturuki
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser alisema waokoaji wapatao 40 kutoka shirika la misaada la Ujerumani (ISAR Ujerumani) walikuwa tayari nchini Uturuki, pamoja na maafisa kadhaa wa jeshi la polisi la shirikisho la Ujerumani. Timu nyingine ya wataalamu kutoka shirika la uokoaji la THW ilichelewa kuondoka Jumanne kwa sababu yahali mbaya ya hewa.
Waturuki wa Ujerumani wakusanya msaada kwa ajili ya wenzao nyumbani
Huko Berlin, vikundi vya jamii vya Waturuki na Wakurdi viliratibu kukusanya, kupanga, na kutuma michango ya misaada kutoka kwa watu wa jamii hizo wanaoishi Ujerumani. Operesheni kama hizo zilikuwa zikiendelea pia Frankfurt na Munich.
Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 25 kutoka mfuko wake wa dharura kwa ajili ya msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mizozo Janez Lenarcic amesema timu 27 za waokoaji kutoka nchi 19 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimepelekwa Uturuki kusaidia. Amesema timu hizo zinajumuisha wataalamu 1150 na mbwa 70 wenye mafunzo ya kunusa.
Vyanzo: msh/wd (AFP, AP, dpa, Reuters)