Trump adai kuna "wizi mkubwa" wakati hesabu zikiendelea
4 Novemba 2020Kura bado zinaendelea kuhesababiwa katika majimbo mbalimbali nchini Marekani na hadi kufikia sasa katika majimbo muhimu Trump amenyakua ushindi kwenye majimbo kama Florida dhidi ya mpinzani wake wa Democrat, Joe Biden. Kadhalika Trump anaongoza Texas, Ohio, Kentucky, Kansas Luisiana, Indiana, Iowa na mengine kadhaa.
Soma pia:Trump na Biden wapelekana bega kwa bega
Kuna majimbo mengine mengi pia yenye ushindali mkali bado ambako bado matokeo hayajatangazwa na macho na masikio yanaelekezwa huko kusubiri nini kitaamuliwa na wapiga kura. Ingawa mgombea wa Democrats Joe Biden ameibuka kidedea kwa mfano katika majimbo ya Arizona, Hawaii, Minessota, Colorado New, Mexico, Carlifornia, New Hampshire, New Jesrsey, Washington, na mengine kadhaa.
Kati ya majimbo 50 tayari mwelekeo wa majimbo 38 umeshajulikana na asubuhi hii macho bado yameendelea kuelekezwa katika majimbo makuu mawili ya Pennsylvania na Michigan ambako ushindani ni mkali baina ya wagombea hao, kiasi cha kuonekana kuanza kuzuka manung'uniko upande wa Trump.
Kadri mambo yanavyozidi kubadilika katika matokeo ya uchaguzi huu Rais Trump ameonesha kuwa na mashaka na mchakato unavyokwenda na saa chache zilizopita alizungumza akiwa ikulu ya White House ambako ameeleza msimamo wake na timu yake.
Trump amesema ataihusisha Mahakama ya Juu ya Marekani akidai kuna wizi wa kura uliofanywa katika matokeo ya uchaguzi huo. Amesisitiza katika tamko lake la leo kwamba anataka shughuli ya kupiga kura kote isimamishwe. Ingawa kwa hakika upigaji kura ulishasimamishwa muda mrefu nchini humo na kinachoendelea ni kuhesabu kura.
Soma pia:Marekani kuchagua rais mpya leo
Kwa upande wake Joe Biden aliyezungumza kabla ya Trump alitowa mwito wa Subra kwa Wamarekani katika shughuli ya kuhesabu kura akitoa pia matumaini kwa wafuasi wake. Biden kadhalika ameshinda ngome ya kusini magharibi ambayo ni jimbo la Arizona, ambalo kiutamaduni ni ngome ya Republican. Ushindi huu umeonesha wazi kuwa pigo kwa Trump.
Hata hivyo, cha kufahamu pia ni kwamba vyombo vya habari ndani ya Marekani vinatofautiana katika utangazaji wa matokeo ya uchaguzi ambapo vingine vinachelewa kutangaza huku vingine vikiwahi kutangaza kwa kuzingatia matokeo ya awali. Kwa mfano katika jimbo la Texas lenye wakaazi milioni 29 baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza matokeo hata kabla kura hazijamaliza kuhesabiwa.
Katika jimbo la Florida timu ya Rais Trump ilitangaza ushindi kwenye ujumbe wa Twitter kabla hata matokeo rasmi. Kinyume na timu ya Trump, timu ya kampeini ya Biden haijawahi kutangaza kupitia Twitter matokeo ya jimbo. Na kinachosisitiza ndani ya Marekani hadi wakati huu ni kwamba bado mshindi hajulikani na kura bado zinaendelea kuhesabiwa.
AFP, AP; Reuters, DPA