Trump aendelea kuteua viongozi wapya wa serikali ijayo
12 Novemba 2024Tajiri huyo wa chama cha Republican mwenye umri wa miaka 78, amemtangaza Tom Homan kama mkuu wa uhamiaji na mipaka, akimtwika jukumu la kutimiza ahadi yake ya kuwatimua wahamiaji wasio na vibali.
Aidha, gazeti la New York Times, limeripoti kwamba Trump anatazamiwa kumteua Seneta wa Florida Marco Rubio kuwa waziri wa mambo ya nje huku Mike Waltz akitajwa kuwa atachukua nafasi ya mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Mike Waltz kuwa mshauri wa Usalama wa Taifa
Wote wawili wamekuwa na mitizamo hasi kuelekea China, ambayo wanaitizama kama tishio na changamoto kwa nguvu za kijeshi na kiuchumi za Marekani.
Trump pia tayari amemteua mbunge wa New York Elise Stefanik kushika wadhifa wa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.