1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump akabiliwa na mashtaka mapya ya nyaraka za serikali

28 Julai 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anakabiliwa na mashtaka mapya ya kumiliki nyaraka zenye siri nzito za serikali huku waendesha mashitaka wakidai aliagiza kufutwa kwa picha za kamera katika makazi yake ya Florida

https://p.dw.com/p/4UUdW
USA Greensboro | Donald Trump bei der North Carolina Republican Party convention
Picha: Chuck Burton/AP Photo/picture alliance

Hati ya mashtaka inajumuisha mashtaka mapya ya kuzuia na kuhodhi kwa makusudi  taarifa za ulinzi wa taifa, hii ikiongezea maelezo mapya kwenye mashitaka yaliyotolewa mwezi uliopita dhidi ya Trump na msaidizi wake wa karibu. Mashtaka hayo ya ziada yalikuja kama mshangao wakati ambapo matarajio yanaongezeka kuhusu uwezekano wa mashtaka ya ziada mjini Washington kuhusu juhudi zake za kubatilisha matokeo ya urais wa uchaguzi wa mwaka 2020.

Madai mapya yanajikita katika kamera ya uangalizi

Madai hayo mapya kutoka kwa wakili maalum Jack Smith yanajikita katika kamera ya uangalizi katika makazi ya Trump ya Mar-a-Lago huko Palm Beach, ushahidi ambao umekuwa muhimu kwa kesi hiyo kwa muda mrefu. Trump anadaiwa kuagiza picha hizo zifutwe baada ya wachunguzi wa idara ya ujasusi na sheria kuzuru eneo hilo mnamo Juni 2022 kukusanya nyaraka hizo zenye siri nzito za serikali alizoondoka nazo baada ya kutoka katika ikulu ya White House. Waendesha mashtaka wanamshutumu Trump kwa kupanga njama na msaidizi wake , Walt Nauta, na msimamizi wa Mar-a-Lago, Carlos De Oliveira, kuficha kanda hiyo ya video kutoka kwa wachunguzi wa serikali baada ya kutoa wito wa kuwasilishwa kwake.

Video yamnasa mfanyakazi wa Trump akihamisha masanduku

Wakili wa utetezi Sasha Dadan na msaidizi wa Trump  Walt Nauta
Wakili wa utetezi Sasha Dadan na msaidizi wa Trump Walt NautaPicha: Rebecca Blackwell/AP/picture alliance

Waendesha mashtaka wamesema video kutoka eneo hilo hatimaye inatekeleza jukumu muhimu katika uchunguzi huo, kwa sababu, waendesha mashitaka wanasema, ilimnasa Nauta akihamisha masanduku ya nyaraka ndani na nje ya chumba cha kuhifadhia bidhaa ikiwa ni pamoja na tukio kama hilo siku moja kabla ya ziara ya Idara ya Sheria katika eneo hilo. Trump pia anashtakiwa kwa kuhodhi  kwa makusudi taarifa za ulinzi wa taifa, zinazohusiana na nyaraka  aliyowaonyesha wageni katika klabu yake ya gofu huko Bedminster, New Jersey, wakati wa mahojiano ya Julai 2021 kuhusu kumbukumbu yake na Mark Meadows ambaye wakati mmoja alikuwa mkuu wa wafanyakazi wake 

Nyaraka ilikuwa mpango wa mashambulizi wa Marekani

Waendesha mashitaka wameelezea nyaraka hiyo kuwa mpango wa mashambulizi wa wizara ya ulinzi ya Marekani na baadaye Meadows, katika kitabu chake, alisema nchi husika ilikuwa Iran. Msemaji mmoja wa Trump amepuuzilia mbali mashtaka hayo mapya na kuyataja kuwa si chochote zaidi ya jaribio linaloendelea la serikali ya Biden la kumnyanyasa Trump na wale walio karibu naye na kushawishi uchaguzi wa urais wa 2024.