Trump akana mashitaka yanayohusiana na uchaguzi
4 Agosti 2023Trump ambaye anaoongoza katika utafiti wa kura za maoni za uteuzi wa wagombea urais kwa mwaka 2024 kupitia tiketi ya chama cha Republican, alikana mashitaka hayo wakati kesi yake ilipokuwa ikisikilizwa kwa takribani dakika 30 katika mahakama ya Washington, ambayo mamia ya wafuasi wake walikutwa na hatia ya kushiriki kwenye ghasia za Januari 6 katika uvamizi wa majengo ya bunge ya Marekani.
"Sina hatia", alisema Trump baada ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo kumsomea mashitaka manne ya jinai na uwezekano wa kifungo jela katika hati ya mashitaka ya kurasa 45 iliyowasilishwa na mwendesha mashitaka maalum Jack Smith. Katika hati hiyo, Smith alimshutumu Trump na washirika wake kwa kuendeleza madai ya uongo kuwa uchaguzi uligubikwa na udanganyifu, kushinikiza maafisa wa majimbo na shirikisho kubadilisha matokeo na kukusanya orodha bandia ya wapiga kura ili kujaribu kupora kura za uchaguzi kutoka kwa Biden.
Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 77 tayari amefunguliwa mashtaka katika kesi nyingine mbili za jinai, huku mashtaka hayo mapya ya kula njama yakiongeza uwezekano wa Trump kuhusishwa zaidi kwenye michakato ya kisheria wakati wa kilele cha kampeni za uchaguzi wa mwaka ujao. Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Reagan kabla ya kuondoka Washington, Trump amesema kuwa kesi hizo zote dhidi yake ni "ukandamizaji wa mpinzani wa kisiasa".
Soma pia: Trump ashtakiwa kwa kujaribu kutengua uchaguzi wa Marekani wa 2020
"Ukiangalia kinachoendelea! haya ni mateso ya mpinzani wa kisiasa. Hii haikupaswa kutokea kabisa Marekani. Kwa hivyo ikiwa huwezi kumshinda, unamtesa au unamfungulia mashtaka. Hatuwezi kuruhusu hili kutokea Marekani," amesema Trump.
Wakili wa Trump, John Lauro, aliwasilisha pingamizi la mapema, akisema kuwa ukubwa wa kesi na kiasi cha nyenzo zinazohusika zinaweza kuhitaji muda mwingi.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa karibu na mahakama ya shirikisho ya E. Barrett Prettyman ambapo kesi hiyo imesikilizwa na kushuhudiwa vizuizi vya chuma na polisi wakishika doria kwenye eneo hilo. Kesi hiyo itasikilizwa tena mnamo Agosti 28.
Hata hivyo, kesi dhidi ya Trump zinaonekana kutokuwa na athari kubwa kama mgombea anayeongoza ndani ya chama cha Republican. Asilimia 47 ya wapiga kura ndani ya chama hicho walisema kuwa wangemuunga mkono katika utafiti wa kura za maoni ulioendeshwa na Reuters na Ipsos baada ya kufunguliwa mashitaka siku ya Jumanne na kumpita gavana wa Florida aliyeshika nafasi ya pili Ron DeSantis.
Vyanzo: Reuters/AFP