Trump alegeza misimamo
23 Novemba 2016Rais mteule wa Marekani Donald Trump anaonekana kulegeza misimamo kuhusu baadhi ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni hasa kuhusu kufutilia mbali mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na kumfungulia mashtaka Bi Hillary Clinton.
Trump aliyefika katika afisi ya shirika hilo la habari na kuhojiwa, amesema anafikiri kunao uhusiano kati ya matokeo ya viwanda na mabadiliko ya tabia nchi, na hivyo anaangalia kwa undani na bongo wazi mikataba iliyotiwa saini kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa mfano mkataba wa Paris. Kauli inayokinzana na wito wake wakati wa kampeni ambapo aliahidi kufutilia mbali mkataba huo na hata kauli yake ya zamani kupitia ukurasa wake wa Twitter ilisema mkataba huo ni Porojo na mbinu ya Uchina kuhakikisha viwanda vya Marekani havifui dafu. Hata hivyo anasema wasiwasi wake ni kujua kwa kiwango gani mikakati inayowekwa itaathiri au itavigharimu viwanda vya Marekani.
Aidha Trump amejitenga na wito wa kumshitaki aliyekuwa mshindani wake Bi. Hillary Clinton akisema anafikiri kufanya hivyo kutazua mgawanyiko zaidi katika nchi. Awali katika kampeni zake, Trump aliahidi kumfungulia Hillary mashtaka kwa madai ya kuharibu rekodi za barua pepe zake kama njia ya kuficha makosa yake na madai ya ufisadi katika wakfu wake. Wito uliokaririwa na wafuasi wake walioimba "Lock her up, lock her up" yaani mfunge Hillary mfunge Hillary.
Kauli nyingine tofauti ya Trump ni kumhusu rais Obama. Trump amesema sasa anampenda hata zaidi Obama hasa baada ya kukutana naye katika ikulu ya White House baada ya ushindi wake na kuwa rais mteule. Awali Trump alisema Obama atakumbukwa kuwa rais mbaya zaidi katika historia ya Marekani.
Hali kadhalika, Trump ameliambia shirika hilo la New York Times kuwa amebadilisha msimamo wake wa kupendekeza mahabusu kupigwa. Hii ni baada ya mazungumzo kati yake na generali mstaafu James Mattis mwisho wa wiki jana ambapo pia walijadili pendekezo la kumteua kuwa waziri wa ulinzi katika serikali yake.
Alipuuzilia mbali kauli ya wanaharakati waliodai kuwa ushindi wake ni wa wale wenye taasubi za uzunguni dhidi ya wengine. Kadhalika alitetea himaya yake ya biashara na kusema hakuna mgongano kati ya himaya hiyo na wajibu wake kama rais.
Sehemu nyingine ambapo Trump ameonekana kulegeza msimamo ni kuhusu kubadilisha sheria za kuchafulia mtu jina ili kuwezesha mashtaka zaidi. Lakini sasa anasema alishauriwa kuwa yeye mwenyewe anaweza kushtakiwa zaidi, jambo analosema hakujua.
Mwandishi: John Juma/APE/AFPE
Mhariri:Josephat Charo