Trump aondoka rasmi ikulu kwa mara ya mwisho kama rais
20 Januari 2021Wasaidizi wa Biden wamesema anatarajia kuanzisha utawala wake kwa kutoa maagizo ya kuirudisha Marekani katika mkataba wa Paris unaohusu mabadiliko ya tabia nchi na pia katika uanachama wa Shirika la Afya Duniani WHO.
Rais mteule wa Marekani Joe Biden anahudhuria maombi katika kanisa, saa chache tu kabla ya kuapishwa kwake.
Rais anayemaliza muda wake Donald Trump ameondoka rasmi katika ikulu ya White House, hivyo kusafisha njia kwa rais mteule Joe Biden kuingia kwenye ikulu hiyo baada ya kuapishwa leo kama rais wa 46 wa Marekani.
Trump hatahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Biden, jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa kisiasa wa nchi hiyo wa kukabidhiana madaraka kwa amani.
Usalama umeimarishwa katika mji wa Washington, huku wanajeshi 25,000 wa kikosi cha Ulinzi wa Taifa wakishika doria pamoja na maafisa wengine wa usalama.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameelezea kushusha pumzi kutokana na kwamba Joe Biden anachukua usukani baada ya Donald Trump, huku akisema kwamba ni siku njema kwa demokrasia. Steinmeier amesema anajua wengi ulimwenguni wanahisi hivyo pia.
Kauli kama hiyo pia imetolewa na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen. Akimpongeza Biden von Der Leyen amesema ujio wa Biden ni uthibitisho kwamba kwa mara nyingine baada ya miaka minne Ulaya ina rafiki katika ikulu ya White House.
Urusi kuhusu mkataba wa New START Biden achukuapo usukani
Nayo Urusi imesema bado imejitolea kuendeleza mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia kati yake na Marekani ujulikanao kama New START, na kwamba itakaribisha juhudi zilizoahidiwa na Biden kufikia makubaliano.
Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba Urusi pamoja na rais wake wanapendelea kuendelezwa kwa makubaliano hayo na kwamba ikiwa Marekani itaonyesha kuwa na nia ya kisiasa kwa haraka kuyaendeleza watakaribisha hatua hizo.
Muda wa mkataba wa New START uliosainiwa 2010 unamalizika mwezi Februari. Mkataba huo unapunguza idadi ya vichwa vya kimkakati vya nyuklia, makombora na mabomu ambayo Urusi na Marekani huweza kutumia.
Wasaidizi wa Biden wamesema katika siku ya kwanza ya utawala wake ataondoa vikwazo ambavyo Trump aliweka dhidi ya watu wanaotoka katika nchi nyingi za Kiislamu. Aidha atasimamisha ujenzi wa ukuta ambao Trump aliamuru kujengwa katika mpaka wa Marekani na Mexico kuzuia uhamiaji wa kinyume cha sheria
Biden kuamuru uvaaji barakoa kwa siku 100 Marekani kwote
Amri nyingine atakayoamuru ni uvaaji barakoa kwa siku 100 katika majengo yote ya serikali ya shirikisho, ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Ikiwa ni pamoja na kubatilisha uamuzi wa Trump wa kuiondoa marekani katika Shirika la Afya Duniani WHO.
Gina McCarthy ambaye ni mshauri mkuu mpya wa Biden kuhusu mabadiliko ya tabia nchi amesema kuirudisha Marekani katika mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu katika kupambana na athari za mabadiliko hayo na ni sera muhimu ya utawala wa Biden.
Biden pia ameahidi kung'oa mizizi ya ubaguzi wa rangi uliojikita kwenye taasisi za nchi hiyo.
China yatarajia kuboreshwa uhusiano na Marekani chini ya Biden
Msemaji wa wizara ya nchi za nje wa China amesema nchi yake inatumai kutakuwa na ushirikiano wenye tija kutoka pande zote mbili. Lakini China italinda masilahi yake, usalama wa taifa na haitapakwa tope na Marekani.
Kauli hizo zimejiri baada ya waziri mtarajiwa wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Anthony Blinken kusema uhusiano wa Marekani na China ni changamoto kuu kwa Marekani.
Iran yataka vikwazo vya Marekani viondolewe chini ya Biden
Kwingineko, rais wa Iran Hassan Rouhani amesema Iran ambayo imekuwa ikizozana na Marekani, iko tayari kufuta tofauti kati yao, lakini yote itategemea uamuzi wa Marekani. Rouhani amesema kile ambacho Marekani itafanya kuhusiana na uhusiano wao, pia watafanya kwa kiwango sawa.
Kuhusu mkataba uliosainiwa mwaka 2015 wa mpango wa nyuklia wa Iran, Rouhani amesema ikiwa Biden ni makini katika kutimiza wajibu wake kimataifa kuhusu Iran, basi Tehran pia itafanya hivyo.
Rais anayeondoka Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye mkataba huo na kuiwekea Iran vikwazo, hatua iliyofuatiwa na Iran kuacha kutimiza ahadi zake za kiufundi kwenye makubaliano hayo.
Rouhani amesema Iran itarudi kutekeleza ahadi zake ikiwa matakwa mengine yataheshimiwa ikiwemo kufuta vikwazo vilivyowekwa.
(AFPE, RTRE, DPAE,)