Trump aridhia kuwa mgombea urais wa Republican
19 Julai 2024Katika hotuba yake ya dakika 90, Trump ametoa ahadi kemkem kwa wapiga kura wake ikiwa ni pamoja na kumaliza migogoro ya kimataifa, kutekeleza operesheni kubwa zaidi ya kuwatimua wahamiaji katika historia ya Marekani.
"Nitamaliza kila mzozo wa kimataifa ambao umeanzishwa na utawala wa sasa, ikiwa ni pamoja na vita vya kutisha kati ya Urusi na Ukraine, ambavyo visingetokea kama ningekuwa rais. Na vita vilivyosababishwa na shambulio dhidi ya Israel, ambalo lisingetokea kama ningekuwa rais." amesema mwanasiasa huyo wa Republican.
Hotuba ya Trump ya kukubali uteuzi, imeashiria kukamilika kwa mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican ambao ulifanyika kwa siku nne.
Akijivunia mafanikio ya kuaminiwa pakubwa na wakereketwa wa chama hicho, Trump ameshuhudia akiimarisha kwenye uchunguzi wa maoni ya umma tangu mdahalo na rais Joe Biden uliofanyika mwezi uliopita. Kwenye mdahalo huo, Biden alipwaya na tangu wakati huo anakabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka aachie ngazi.
Trump aonesha kuimarika hata kwenye ngome za chama cha Democratic
Kampeni ya Trump imekuwa ikizungumza hata uwezekano wake kupenya katika majimbo yaliyo ngome za chama cha Democratic kama vile Minnesota na Virginia.
Wakati Trump anazidi kujiamini kurejea kwa njia ya kushangaza katika Ikulu ya White House, licha ya matatizo mengi ya kisheria na mashitaka mawili yaliyougubika muhula wake wa kwanza, Rais Joe Biden anakabiliwa na anguko kubwa la umaarufu wake na wasiwasi wa chama chake kuhusu afya yake.
Akiwa na umri wa miaka 81, Biden amekuwa akikabiliwa na miito inayoongezeka kutoka chama chake kujiengua kwenye uchaguzi kutokana na wasiwasi wa umri wake, na wiki yake ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kugunduliwa na maambukizo ya virusi vya UVIKO-19.
Trump mwenyewe alidhoofika baada ya kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2020 na ghasia zilizofanywa na wafuasi wake dhidi ya majengo ya bunge, lakini ametumia muda mrefu wa miaka minne iliyopita kuunda upya siasa za Republican.
Akiweka wafuasi waaminifu, akiwemo mke wa mtoto wake Lara Trump katika uongozi wa Kamati ya Taifa ya chama cha Republican, tajiri huyo kimsingi amezima upinzani wowote ndani ya chama.