Truss afanya kikao chake cha kwanza na timu yake ya mawaziri
7 Septemba 2022Truss, ambaye aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza jana Jumanne baada ya kukutana na Malkia Elizabeth nchini Scotland kufuatia kujiuzulu kwa Boris Johnson, anatazamiwa kukutana na timu yake kuu katika mkutano wa asubuhi.
Timu hiyo inajumuisha mchanganyiko wa watu mbalimbali kuwahi kutokea katika historia ya Uingereza wakiwemo Kwasi Kwarteng, Waziri wa fedha, James Cleverly Waziri wa mambo ya nje na Suella Braverman, Waziri wa mambo ya ndani.
Soma pia: Mfahamu Liz Truss na safari yake kisiasa
Timu yake hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu, haswa juu ya mfumuko wa bei na jinsi ya kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha kwani bei za nishati zinatarajiwa kupanda kwa hadi asilimia 80 kuanzia mwezi ujao na kisha kupanda tena mnamo mwezi Januari.
Benki Kuu ya Uingereza imetabiri kuwa nchi hiyo itashuhudia mdororo wa kiuchumi baadaye mwaka huu.
Bi Truss pia ametwikwa jukumu la kushughulikia mipango ya biashara ya nchi hiyo baada ya Brexit katika kisiwa cha Ireland ya Kaskazini, na katika moja kati ya mazungumzo yake ya kwanza kwa njia ya simu jana jioni, alikubaliana na Rais wa Marekani Joe Biden kuhusu umuhimu wa kulinda amani Ireland ya Kaskazini, ambayo ni sehemu ya Uingereza.
Katika taarifa yake, Ikulu ya White House imeongeza kuwa Truss na Biden pia walizungumzia juu ya changamoto zinazoletwa na China na kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
Soma pia: Kutoka Brexit hadi Partygate, hatimaye Johnson ajiuzulu
Licha ya changamoto lukuki zinazomkabili Waziri Mkuu huyo mpya wa Uingereza, ameonyesha matumaini kuwa ana uwezo wa kuzikabili wakati alipoingia kwenye ofisi yake iliyoko katika mtaa wa Downing Street, mjini London. Amesema "Nina Imani kwamba kwa Pamoja tunaweza kuondokana na dhoruba hii inayotukabili.”
Kupunguzwa kwa ushuru na kulekeza ufadhili zaidi katika sekta ya uhifadhi wa jamii huenda ikawa miongoni mwa ajenda kuu ya mkutano huo wa leo.
Bi Truss aidha ameahidi kupunguza ushuru na kuongeza ukuaji wa biashara na uwekezaji. Ameapa kulitazama kwa jicho la karibu suala la bili za umeme na gesi na kwa ujumla suala la sera ya nishati.
Baada ya mkutano huo wa baraza la mawaziri, Truss atasafiri hadi bunge la Commons katika kikao cha maswali na majibu na kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour Keir Starmer.