1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuchel: Hatukujiandaa vizuri dhidi ya Frankfurt

11 Desemba 2023

Rekodi ya Bayern Munich ya kutofungwa msimu huu katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga imeota mbawa baada ya kupokea kichapo cha 5-1 mbele ya Eintracht Frankfurt uwanjani Deutsche Bank Park.

https://p.dw.com/p/4a1X4
Bundesliga | Mechi ya mzunguko wa 14 | Eintracht Frankfurt vs. FC Bayern München
Kiungo wa Eintracht Frankfurt Hugo Larsson akisherehekea baada ya kufunga bao la tatu dhidi ya Bayern MunichPicha: Michael Bermel/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Mshambuliaji raia wa Misri Omar Marmoush alikuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Bayern na aliisaidia timu yake kumaliza msururu wa kufungwa mechi nne mfululizo katika michuano yote. Marmoush, sasa amefunga mabao saba ndani ya ligi.

Kadhalika, nyota wa Bayern Munich Harry Kane ameingia kwenye rekodi kwa kupoteza mchezo wake wa kwanza akianza kama mshambuliaji, na wa pili katika soka lake la Ujerumani kwa ujumla.

Pia ilikuwa mara yake ya tatu kwa nahodha huyo wa timu ya taifa ya England kutofunga bao katika michezo 13 ya Bundesliga.

Soma pia: Terzic: Tulifanikiwa kuwadhibiti Leverkusen kimbinu

Baada ya kichapo hicho, mkufunzi wa Bayern Munich Thomas Tuchel amesema walistahili kupoteza mechi hiyo.

"Lazima niwe mkweli, imekuwa siku mbaya ofisini, hilo halina mjadala. Ni vigumu kueleza kilichotokea baada ya wiki moja ya mazoezi. Hatuna sababu ya kujitetea kwa jinsi tulivyocheza leo. Sijawahi kuhisi hivi lakini inaonyesha tulikosa umakini na kuruhusu mabao rahisi. Ilikuwa rahisi sana kwao kufunga licha ya nafasi finyu waliokuwa nayo. Kwa ujumla, hatukuwa tayari kwa mchezo wa leo, na hilo ni kosa letu wenyewe."

Kufungwa kwa Bayern Munich kumeiacha Bayer Leverkusen kuwa timu pekee ambayo bado haijapoteza mechi yoyote kufikia sasa.

Kipigo hicho pia hakikutarajiwa kwani Frankfurt ilikuwa imepoteza mechi nne mfululizo ikiwemo kipigo katikati ya wiki mbele ya timu ya daraja la tatu ya Saarbrucken katika Kombe la DFP Pokal.

Mkufunzi wa Eintracht Frankfurt Dino Toppmöller amesema "Ninajivunia sana timu hii. Wameonyesha ari katika michezo yote - isipokuwa michezo miwili iliyopita - uwezo wao na hamu ya kutaka ushindi. Imenipa faraja. Ushindi wa leo ni mzuri kwetu sote kwa sababu tuliteseka wiki za nyuma, na tulihitaji kuonyesha mchezo mzuri."

Leverkusen haijapoteza mechi 22 katika mashindano yote inayoshiriki

Ligi Kuu ya kandanda ya Bundesliga | VfB Stuttgart vs Bayer 04 Leverkusen
Wachezaji wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz na Victor BonifacePicha: Langer/IMAGO

Na katika dimba la MHP Arena, mjini Stuttgart kiungo Florian Wirtz alifunga bao la kusawazisha kunako dakika ya 47 ya mchezo na kuisaidia klabu yake ya Bayer Leverkusen kuondoka na alama moja muhimu dhidi ya wenyeji Stuttgart na hivyo kuendeleza rekodi ya kutofungwa msimu huu.

Vijana wanaotiwa makali na Xabi Alonso wamesalia kileleni mwa Bundesliga wakiwa na alama 36, alama nne mbele ya miamba Bayern Munich japo wana mechi moja kibindoni. Hii ni baada ya mechi yao dhidi ya Union Berlin kuahirishwa wiki iliyopita kutokana na kumwagika kwa theluji uwanjani.

Soma pia: Bayer Leverkusen wapo kileleni mwa Bundesliga wakiwa na alama 22

Baada ya kutoka sare katika mechi mbili mfululizo za Bundesliga, mshambuliaji wa Bayer Leverkusen Victor Boniface amesema, "Tumetoka sare dhidi ya timu mbili mahiri, Dortmund na Stuttgart. Nahisi tunaweza kupata matokeo bora zaidi ila sasa nguvu zetu tunazielekeza kwenye mchezo ujao nyumbani."

Kwengineko, Borussia Dortmund iliangukia pua mbele ya RB Leipzig katika dimba la Signal Iduna Park kwa kufungwa mabao 3-2 na kuzima ndoto yao ya kuwania ubingwa wa Bundesliga msimu huu.

Masaibu ya Dortmund yalianza mapema kunako dakika ya 15 ya mchezo baada ya beki mzoefu Mats Hummels kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Lois Openda.

Ushindi wa RB Leipzig umeipandisha hadi katika nafasi ya nne, wakiwa na alama 29, alama mbili tu nyuma ya VfB Stuttgart iliyokamata nafasi ya tatu.